IQNA

Polisi Nigeria washambulia Waislamu wa madhehebu ya Shia, wanne wajeruhiwa

22:07 - November 04, 2016
Habari ID: 3470651
IQNA-Watu wanne wamejeruhiwa baada ya polisi nchini Nigeria kuwashambulia Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa wakiandamana Ijumaa ya leo katika mji mkuu Abuja.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, maandamano hayo ya amani yameitishwa kuitaka serikali kumuachulia huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye anashikiliwa akiwa pamoja na mke wake pamoja na wafuasi wake kadhaa.

Wakati huo huo, Waislamu wa madhehebu ya Shia huko Nigeria wamekosoa vikali ukandamizaji unaofanywa dhidi yao na vyombo vya usalama nchini humo na kusisitiza kuwa, dhulma hizo zimetokana na fikra za Kiwahabi. Abdul Giwa, msemaji wa Harakati ya Kiislamu Nigeria amesema vyombo vya dola vimeanzisha 'kampeni ya umwagaji damu na uharibifu' dhidi ya Mashia wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, na kwamba harakati hizo zimechochewa na idiolojia ya Uwahabi ambayo chimbuko lake ni Saudi Arabia.

Giwa ameliambia shirika la habari la Reuters kama tunavyomnukuu: "Tuna uhuru na haki ya kuabudu, kinachotakiwa kufanywa na serikali ni kutudhaminia usalama, kutuelewa na kutotuhujumu."

Ikumbukwe kuwa kati ya Disemba mwaka 2015, Jeshi la Nigeria liliwashambulia wafuasi wa Harakati ya Kiislamu Nigeriakatika mji wa Zaria jimboni Kaduna kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Jeshi hilo lilidai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Allamah Sheikh Ibrahim Zakzaky walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo. Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ni mahututi, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.

captcha