IQNA

Serikali ya Nigeria yatakiwa na mahakama imuachilie huru Sheikh Zakzaky

18:56 - December 02, 2016
Habari ID: 3470709
IQNA-Serikali ya Nigeria imeiamuriwa na mahakama kumuachilia huru mara moja Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Katika hukumu iliyotolewa leo Ijumaa, Jaji Gabriel Kolawole wa Kitengo cha Abuja cha Mahakama Kuu ya Nigeria ameiamuru serikali kumuachilia huru Sheikh Zakzaky na mke wake katika kipindi cha siku 45.

Jaji huyo ameonya kuwa, iwapo Sheikh Zakzaky atapoteza maisha akiwa gerezani, jambo hilo linaweza kuibua ghasia na kupelekea idadi kubwa ya watu kupoteza maisha.

Sheikh Ibrahim Zakzaky amekuwa akishikiliwa na vyombo vya usalama vya Nigeria kwa karibu mwaka mmoja sasa bila ya kufunguliwa mashtaka hatua ambayo imekuwa ikilalamikiwa na taasisi za kutetea haki za binadamu.

Tangu mwaka uliopita hadi sasa harakati ya Kiislamu Nigeria na wafuasi wake wamekuwa wakikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa serikali ya nchi hiyo.

Miezi 11 iliyopita, yaani Desemba mwaka jana, Jeshi la Nigeria liliwashambulia wafuasi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria katika mji wa Zaria jimboni Kaduna kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Jeshi hilo lilidai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Allamah Sheikh Ibrahim Zakzaky walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo. Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ni mahututi, akiendelea kushikiliwa korokoroni.

550309

captcha