IQNA

Msikiti wa Muhammad Rasulullah (SAW) katika mji mkuu wa Iran, Tehran uko katika eneo lenye ukubwa wa mita mraba 1,000 na ujenzi wake ulifadhiliwa na Bwana Ali Akbar Ansari. Msikiti huu una ukumbi wake mkuu wa Sala wenye sehemu maalumu ya wanawake na ya wanaume na kuna ghorofa mbili za kituo cha kufunza Qur'ani Tukufu maarufu kama Darul Qur'an. Aidha msikiti huo una maktaba na pia eneo la jikoni.

Moja ya vivituio vya msikiti huu ni usanifu majengo wake unaoshabihiana na ule wa Al-Masjid an-Nabawī katika mji wa Madina kwa mtazamo wa qubaa na nguzo zake. Aidha baadhi ya nukta za usanifu majengo wa msikiti huo zinashabihiana na za Msikiti wa Jamia wa mji wa Isfahan nchini Iran. Kivutio kingine katika msikiti huu ni  zulia moja kubwa ambalo halijaunganishwa lililo katika ukumbi mkuu wa Sala. Halikadhalika msikiti  huo pia una shandalia (chandelier) ambazo huwa na nuru yenye mvuto mbali na mapambano mengine yanayoshabihiana sana na yale yaliyo katika Al-Masjid an-Nabawī .

Ikumbukwe kuwa tarehe 21 mwezi Agosti ni maadhimisho ya kuchomwa moto na Wazayuni msikiti wa al Aqsa miaka 50 iliyopita yaani mwaka 1969. Kufuatia pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu, OIC, imeitangaza siku hii kuwa Siku ya Kimataifa ya Misikiti.