IQNA

Haram Takatifu ya Imam Ali katika Siku ya 13 ya Rajab

TEHRAN (IQNA) – Baada ya maandalizi kama vile kusafisha, kuosha na kupamba kwa maua, kaburi tukufu la Imam Ali (AS) huko Najaf, Iraq, limekuwa uwanja wa sherehe siku ya Ijumaa na leo, ambayo ni siku ya 13 ya mwezi wa Rajab katika Hijria Qamari na inaashiria kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Imam wa kwanza wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia (AS).

Siku kama ya leo miaka 1467 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa katika nyumba tukufu ya al Kaaba, Ali bin Abi Twalib AS, ambaye ni binamu, mkwe na Khalifa wa Mtume Muhammad (saw). Mama wa mtukufu huyo ni Bibi Fatima bint Assad na baba yake ni Abu Talib. Katika kipindi chake cha utotoni, Ali bin Abi Talib alilelewa na kupata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu SAW, na alikuwa mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu. Mwishoni mwa mwaka wa Pili Hijria, Imam Ali AS alimuoa Bibi Fatimatul Zahra binti ya Mtume Mtukufu SAW. Imam Ali AS alishiriki kwenye vita vyote bega kwa bega na Mtume Mtukufu SAW isipokuwa vita vya Tabuk, na alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume katika hali zote za shida na matatizo. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji asiye na mithili, lakini Imam Ali bin Abi Talib alikuwa mpole, mwingi wa huruma na mtetezi wa wanyonge.