IQNA

Maombolezo ya Fatima Zahra (AS) yafanyika Zambia

11:21 - May 13, 2009
Habari ID: 1777628
Hafla za maombolezo ya Bintiye Mtume (SAW), Bibi Fatima Zahra (AS) yaani ‘Siku za Fatimiya’ zimefanyika hivi karibuni nchini Zambia kwa usimamizi wa Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini humo.
Hafla zilianza Alhamisi wiki iliyopita katika Msikiti wa Imam Redha (AS) katika mji kuu wa Zambia Lusaka. Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA nchini Zambia, halfa hizo zimekuwa zikifanyika kila siku baada ya Sala za Magharibi na Isha’a na programu huanza kwa tilawa ya Quran Tukufu na tafsiri yake. Khatibu katika hafla hizo ni Sheikh Asadi Muwahidi Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Zambia ambaye hutoa mhadhara kuhusu fadhila za Bibi Fatima Zahra (AS).
Katika hotuba yake Alhamisi iliyopita, Sheikh Muwahidi aliashiria nafasi ya Bibi Zahra (AS) katika historia ya Uislamu na kusema: “Hakuna sahaka kuwa Fatima Zahra (AS) ni mwanamke apendwayo zaidi na Waislamu na wasiokuwa Waislamu kutokana na sifa zake za kidini, kielimu, kifasihi, kitaqwa (uchaji Mungu) na maadili. Bibi Fatima Zahra (AS) ni kigezo kwa wanawake wote wapendao heshima na fadhila.
Amesema kuwa, ni katika utakasifu wa Bibi Fatima Zahra (AS) ndio waliibuka shakhsia wawili wa kipekee ulimwenguni ambao ni Imam Hassan (AS) aliyekuwa dhihirisho la heshima na subira na Imam Hussein (AS) kiongozi wa Mashahidi. Aidha Zainab Kubra (AS) pia alilelewa na mikono mitakatifu ya Bibi Fatima Zahra (AS).
Sheikh Muwahidi amekumbusha kuwa Mtume (SAW) alisema Bibi Fatima Zahra (AS) ni ‘Kiongozi wa Wanawake wote Duniani’. 403978
captcha