IQNA

Matamshi ya Kiongozi Muadhamu katika Mkutano wa 16 wa Viongozi wa Harakati ya NAM

23:27 - August 31, 2012
Habari ID: 2402214
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Alkhamisi 30 Agosti amehutubia kikao cha ufunguzi wa mkutano wa Wakuu wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM mjini Tehran na kubainisha mabadiliko yanayotokea katika mfumo wa kimataifa. Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba hiyo.
Bismillahir Rahmanir Rahim
Hamdu zote zinamstahikia Allah, Mola Mlezi wa viumbe pia. Na rehema na amani zimwendee Bwana Mtume Mtukufu na Mwaminifu na Aali zake watoharifu na masahaba wake wateule na Manabii na Mitume wote.
Kwanza kabisa ninakurabirisheni kwa mapana na marefu wageni wetu wapendwa, viongozi na wajumbe wote mnaowakilisha nchi mbali mbali duniani wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM na washiriki wengine kwenye mkutano huu wa kamataifa. Tumekusanyika hapa ili - kwa muongozo na msaada wa Mwenyezi Mungu - tuweze kuiendeleza harakati hii ambayo ilianzsishwa karibu miongo sita iliyopita kwa muono wa mbali na utambuzi wa kina na wa kishujaa wa viongozi kadhaa wa kisiasa wenye uchungu na mataifa ya dunia na wanaojua vizuri kutekelea majukumu yao. (tuekusanyika pamoja hapa), ili tuifanye harakati hii ya NAM iendelee kulinganana na mahitaji na mazingira yalivyo duniani leo na tuweze pia kuipa uhai mpya. Wageni wetu waliokusanyika hapa kutoka katika maeneo tofauti ya kijiografia ya mbali na ya karibu na wanaotoka kwenye mataifa na vizazi tofauti na wenye itikadi, mila, historia na turathi tofauti kabisa, lakini pamoja na hayo, wote wamekusanyika hapa kama alivyowahi kusema Ahmed Sukarno, mmoja wa waasisi wa harakati hii katika mkutano maarufu wa Bandong mwaka 1955 kwamba, msingi wa kuasisiwa harakati ya NAM si kuziunganisha nchi kijiografia au kitaifa au kidini, bali ni kwa ajili ya kuunganisha mahitaji ya mataifa wanachama. Yale mambo ambayo yalikuwepo wakati wa kuasisiwa kwake harakati ya NAM na kuyafanya mataifa wanachama yaungane ili kujiepusha na udhibiti wa kanali zenye nguvu za kibeberu, mambo hayo bado yapo leo hii, tena katika mazingira ambayo mabeberu wamezifanya za kisasa kabisa mbinu zao za kukandamiza mataifa mengine.
Hapa ninapenda kuzungumzia uhakika mwingine kama ifuatavyo:
Uislamu umetufunza kwamba wanaadamu wote licha ya kutofautiana vizazi, lugha na tamaduni zao lakini wana maumbile mamoja ambayo yanawataka wawe wasafi, waadilifu, wema, wahurumiane na washirikiane na ni maumbile hayo ya wanadamu wote ndiyo yanayomuwezesha kiumbe huyu kuvuka salama kwenye mambo yanayomsukuma kwenye upotofu, na ni maumbile hayo ndiyo yanayomvuta mwanadamu kwenye tauhidi na kutambua dhati tukufu ya Mwenyezi Mungu.
Uhakika huo unaong'ara ni mpana kiasi kwamba una uwezo wa kuweka misingi madhubuti ya kuundika jamii huru yenye fakhari na vitu vingi vya kujivunia katika upande wa maendeleo na uadilifu sambamba na kumimina nuru ya umaanawi ndani ya kazi zote za kimaada na kidunia za wanaadamu na kumtunuku binadamu pepo ya dunia kabla ya pepo ya Akhera iliyoahidiwa na dini zote za Mwenyezi Mungu. Na ni uhakika huu wa pamoja na wa wote ndio unaoweza kuweka misingi madhubuti ya ushirikiano wa kidugu kati ya mataifa yote ya dunia hata kama ukiuangalia kijuu juu muundo wa kihistoria, kijiografia na kieneo wa mataifa hayo utaona mataifa hayo hayafanani hata kidogo.
Wakati wowote ushirikiano wa kimataifa unaposimama juu ya msingi huo - katika mahusiano ya mataifa hayo - tawala na serikali mbali mbali za dunia haziwezi kusalitiana wala kujiuza kwa mataifa mengine kutokana na woga, vitisho, au kupenda makubwa na manufaa ya upande mmoja au ya kibeberu, bali uhusiano wao husimama juu ya msingi wa manufaa salama na ya pamoja na bora kuliko yote na utajengeka juu ya msingi wa mahitaji ya kibinaadamu na kuzipa utulivu nafsi za wanadamu pamoja na kuziweka salama fikra na akili za mataifa yao mbele ya matatizo mengi yanayozikabili.
Mfumo huu ambao kila mtu anatamani uwepo, umesimama katika mkabala wa mfumo wa kibeberu ambao kwa karne nyingi ulikuwa unapigiwa propaganda na kuendeshwa na madola ya kibeberu ya Maghabiri na hivi sasa serikali ya kibeberu na ya kivamizi ya Marekani iko mstari wa mbele katika kuuendeleza, kuuongoza na kuuendesha mfumo huo wa kibeberu.
Wageni wetu wapendwa!
Leo hii malengo makuu ya Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM baada ya kupita miongo 6 ya kuasisiwa kwake bado yako hai na ni imara. Malengo kama vile kupambana na ukoloni na kupigania uhuru wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni yameifanya harakati ya NAM kuwa kambi yenye nguvu na kuwa chombo cha kuimarisha mshikamano na ushirikiano kati ya nchi zote wanachama. Kwa kuangalia hali ilivyo hivi sasa duniani itaonekana kuwa ni jambo lililo mbali kufanikishwa malengo hayo lakini popote palipo na nia ya kweli na juhudi za pande zote za kufikia kwenye malengo makuu yaliyo magumu kufikiwa, basi nia na juhudi hizo huyaletea matumaini mataifa na hatimaye kuyapa matunda mazuri, hata kama kutakuwa na changamoto nyingi katika njia ya kufikia huko.
Sisi katika kipindi si cha zamani sana tumeshuhudia kushindwa siasa za kipindi cha vita baridi na baada ya hapo tumeshuhudia pia kushindwa kipindi cha siasa za kila nchi kujifanyia mambo kivyake. Baada ya kupata funzo, tajiriba na uzoefu huo wa kihistoria, hivi sasa dunia imo katika kipindi cha kuelekea kwenye mfumo mpya wa kimataifa na kwamba Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM inaweza bali inapaswa kutoa mchango mkubwa na mpya katika suala hilo. Mfumo huo mpya wa kimataifa unapaswa usimame juu ya msingi wa kuyashirikisha mataifa yote na kwa usawa na kwamba mshikamano wetu sisi nchi wanachama wa harakati hii ni jambo la dharura na muhimu sana kwa ajili ya kuundika mfumo huo katika zama hizi.
Kwa bahati nzuri mambo yanayojiri hivi sasa duniani yanatoa bishara njema ya kuundika mfumo wa pande kadhaa ambao ndani yake kambi za jadi za madola makubwa zinaondoka na nafasi yake kuchukuliwa na majimui na kundi la nchi zenye tamaduni na ustaarabu wa kila namna na zenye miundo tofauti ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Matukio ya kipekee tuliyoyashuhudia katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita yanaonesha wazi kuwa kujitokeza juu madola mengi mapya kunakwenda sambamba na kudhoofika madola makubwa ya zamani. Uguraji huu wa pole pole wa madaraka unazipa fursa nchi wanachama wa NAM kutoa mchango mkubwa na wenye taathira nzuri kimataifa na kuandaa mazingira ya kuweko uongozi wa kiadilifu na wa kuyashirikisha kikamilifu mataifa yote katika maamuzi ya dunia hii pana.
Sisi nchi wanachama wa harakati hii tumeweza katika kipindi kimoja kirefu na licha ya kuweko mitazamo na mielekeo tofauti, kulinda mshikamano na umoja wetu ndani ya mipaka ya malengo matukufu ya pamoja na haya si matunda madogo wala si kitu kilichopatikana kirahisi. Mshikamano huu unaweza kuwa dira ya mfumo mpya uliosimama juu ya misingi ya uadilifu na ubinaadamu.
Hali iliyojitokeza duniian leo hii ni fursa ambayo huenda harakati ya NAM isiipate tena. Tunayosema sisi ni kuwa, usukani wa dunia haupaswi kuwa mikononi mwa nchi chache za kidikteta za Magharibi. Inabidi kuundike mfumo utakaoweza kuyashirikisha kidemokrasia mataifa yote ya dunia katika uendeshaji wa masuala ya kimataifa na kuwadhaminia walimwengu jambo hilo. Haya ndiyo mambo ambayo mataifa yote ya dunia yana hamu nayo; mataifa ambayo kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja yamepata madhara kutokana na ubeberu wa nchi chache zinazopenda kutawala mataifa mengine duniani.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina muundo na mfumo usio wa kimantiki na ambao si wa kidemokrasia hata kidogo bali mfumo wake ni udikteta wa waziwazi na ni mfumo ulipitwa na wakati, ni wa kizamani na ni ambao hauna nafasi tena katika dunia ya leo. Ni kwa kutumia muundo huo ghalati na mbovu ndio maana Marekani na washirika wake wanaopenda kuzifanyia ubeberu nchi nyingine wakawa wanatumia vibaya istilahi mbali mbali tukufu kwa ajili ya kuibebesha dunia siasa zao. Utazisikia nchi hizo za kibeberu zikizungumzia "haki za binaadamu" wakati kumbe zinakusudia maslahi na manufaa ya Magharibi, zinazungumzia "demokrasia" na kutumia istilahi hiyo kuingilia kijeshi katika nchi nyingine; zinazungumzia "kupambana na ugaidi" na kutumia jambo hilo kujaribishia silaha zao kwa kuwamiminia mawimbi ya mabomu na mashambulizi watu wasio na ulinzi wa vijijini na katika miji ya mataifa mengine. Kwa mtazamo wa madola hayo, ubinadamu unagawanyika katika mafungu matatu, wanadamu wa daraja la kwanza, wa daraja la pili na wa daraja la tatu. Roho za wanadamu wa Asia, Afrika na Amerika ya Latini ni rahisi lakini thamani ya roho za watu wa Marekani, Magharibi na Ulaya ni ya juu. Usalama wa Marekani na Ulaya ni muhimu lakini usalama wa wanadamu wengine inadaiwa hauna umuhimu. Kama mateso na mauaji yatafanywa na Marekani, na Wazayjni na vibaraka wao yanahesabiwa ni jambo la sawa na linalofumbiwa macho kikamilifu. Katika jela zao za siri zilizoko katika maeneo mengi ya mabara tofauti ya dunia kunashuhudiwa vitendo vya kinyama, vya aibu na viovu mno dhidi ya wafungwa wasio na ulinzi wala wakili wa kuwatetea na wala mahakama za kusikiliza kesi zao huku roho za wanaofanya unyama huo zikiwa hazitetereki hata kidogo. Mambo yote mazuri na mabaya yanaangaliwa kiubaguzi kikamilifu na kwa kuzingatia nchi na nchi. Wanayalazimisha mataifa ya dunia kuamini kuwa "sheria za kimataifa" ni kulinda manufaa ya madola hayo ambayo yanahalalisha matamshi yao ya kibeberu na yasiyokubalika kisheria kwa kuyabandika jina la "jamii ya kimataifa." Madola hayo ya kibeberu yanatumia ukiritimba wa vyombo vyao vya habari kuufanya uongo uonekane ukweli na kutangaza masuala yote ya haki kuwa ni uasi.
Ndugu wapendwa! Hali hii iliyojaa makosa na madhara mengi haipaswi kuendelea. Watu wote wameshachoshwa na mfumo huu ghalati wa kimataifa. Harakati ya Asilimia 99 ya wananchi wa Marekani dhidi ya taasisi za matajiri na zenye udhibiti wa kila kitu nchini humo na maandamano makubwa ya wananchi katika nchi nyingine za Ulaya Magharibi dhidi ya sera za kiuchumi za tawala zao pia ni mambo yanayoonyesha kujaa na hadi kufurika kipimo cha subira na uvumilivu wa wananchi wa nchi hizo. Kwa kweli inabidi kuitafutia tiba hali hii isiyokubalika.
Mshikamano madhubuti na wa kimantiki na wa pande zote wa nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizisofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM unaweza kutoa mchango mkubwa katika juhudi za kutafuta na kuendelea na njia ya kutibu hali hiyo.
Amani na usalama wa kimataifa ni miongoni mwa masuala muhimu mno katika dunia yetu ya leo na kupambana na silaha za mauaji ya umati na zenye kuleta maafa kwa mwanadamu ni moja ya mambo ya dharura na yanayohitajika haraka sana kwa mataifa yote leo hii. Katika dunia ya leo, usalama ni suala linaloyahusu mataifa yote na si sahihi kufanya ubaguzi katika jambo hilo. Zile nchi ambazo zimejilimbikizia silaha za mauaji ya umati katika maghala yao, hazina haki ya kudai kuwa ni wabeba bendera ya kupigania usalama na amani ya kimataifa. Hili - bila ya shaka yoyote haliwezi hata kuzidhaminia usalama nchi hizo zenyewe. Kwa masikitiko makubwa leo hii inashuhudiwa kuwa, nchi zinazomiliki silaha nyingi zaidi za nyuklia hazina hamu yoyote ya kuondoa silaha hizo angamizi katika mifumo yao ya ulinzi na ya kijeshi bali zinatumia silaha hizo kama wenzo wa vitisho na kujikweza kisiasa na kimataifa. Mtazamo huo haukubaliki hata chembe na ni kitu cha kutupiliwa mbali.
Silaha za nyuklia si kitu cha kudhamini usalama na wala si kitu cha kuliletea taifa nguvu za kisiasa bali ni tishio kwa mambo yote hayo mawili. Matukio ya muongo wa 90 wa karne ya ishirini yamethibitisha kwamba kuwa na silaha hizo hakuwezi kuulinda utawala hata kama wa Urusi ya zamani. Leo hii pia tunazijua nchi ambazo zinakabiliwa na machafuko mengi na mabaya sana licha ya kuwa na mabomu ya atomiki.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakuhesabu kutumia silaha za nyuklia, za kemikali na silaha nyinginezo kama hizo kuwa ni madhambi makubwa yasiyosameheka. Sisi tumebuni kaulimbiu ya "Mashariki ya Kati bila ya Silaha za Nyuklia" na tumeshikamana vilivyo na kaulimbiu hiyo. Hii haina maana kabisa ya kupinga matumizi ya njia za amani ya nishati ya atomiki na uzalishaji wa fueli nyuklia. Kustafidi kwa njia za amani na nishati hiyo, kulingana na sheria za kimataifa, ni haki ya nchi zote duniani. Nchi zote zinapaswa kuwa na uwezo wa kutumia nishati hiyo salama katika mambo mbali mbali muhimu ya nchi na mataifa hayo, na kuzifanya nchi hizo zisilazimike kuwa tegemezi kwa nchi nyingine katika kustafidi na haki yao hiyo. Nchi chache za Magharibi ambazo zenyewe zinamiliki silaha za nyuklia na zinakwenda kinyume na sheria kwa kitendo chao hicho, zina hamu ya kuona zinadhibiti pia uwezo wa kuzalisha fueli nyuklia. Hivi sasa kumeanza kuundika harakati yenye kutia shaka ya kudhibiti uzalishaji na uuzaji wa fueli nyuklia kutoka kwa vituo vinavyodaiwa vya kimataifa wakati uhakika wake ni vituo vya nchi chache tu za Magharibi na kunafanyika juhudi za kuligeuza jambo hilo kuwa la kudumu.
Kichekesho kichungu cha zama zetu hizi ni kwamba, serikali ya Marekani ambayo ndiyo inayomiliki silaha nyingi zaidi hatari za nyuklia na silaha nyinginezo za mauaji ya umati na ambayo ndiyo nchi pekee iliyowahi kutumia silaha hizo katika historia ya mwanadamu, leo hii inataka kuwa kiranja wa kukabiliana na uenezaji wa silaha za nyuklia! Wamarekani na mashirika yao ya Magharibi yameupa utawala ghasibu wa Kizayuni silaha za atomiki na kulitumbukiza eneo hili nyeti kwenye hatari kubwa lakini nchi hizo hizo danganyifu ndizo zinazokuwa wakali sana zinapoona nchi huru duniani zinataka kustafidi kwa njia za amani na kwa malengo ya kiraia na nishati ya nyuklia. Nchi hizo zinapinga kwa nguvu zao zote, hatua ya nchi huru dunia ya kuzalisha fueli nyuklia kwa ajili ya kuzalisha dawa za mionzi na matumizi mengine ya amani na ya kibinaadamu. Kisingizio na madai ya uongo yanayotolewa na madola hayo ni kuogopa uzalishaji wa silaha za atomiki. Madola hayo yenyewe yanajua vyema kuwa yanasema uongo kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika suala hilo. Hata hivyo misimamo ya kisiasa ya madola hayo ambayo hayana chembe ya athari za umaanawi inayafanya yahalalilshe kusema na kukubali uongo kirahisi sana. Je zile nchi ambazo katika karne ya ishirini na moja zinatumia vitisho vya kutumia silaha za nyuklia tena bila ya hata kuona haya, zinaweza kweli kujiepusha au kuona haya kusema uongo kama huo?!
Hapa ninapenda kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu kamwe haijawahi kufuatilia suala la kumiliki silaha za nyuklia kama ambavyo pia kamwe haitafumbia jicho haki ya taifa lake ya kustafidi kwa njia za amani na nishati ya atomiki. Kaulimbiu yetu ni "Nishati ya Nyuklia kwa ajili ya Wote na Silaha za Nyuklia Si kwa Yeyote." Tutaendelea kutilia mkazo masuala yote hayo mawili (mosi haki ya watu wote kuwa na haki ya kustafidi na nishati ya nyuklia na pili mtu yeyote asiruhusiwe kumiliki silaha za nyuklia) na tunajua kuwa, kuondoa ukiritimba na udhibiti wa nchi chache za Magharibi wa uzalishaji wa nishati ya nyuklia katika mipaka ya Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia ni kwa faida ya nchi zote huru zikiwemo nchi wanachama wa harakati ya NAM.
Uzoefu wa miongo mitatu ya kusimama imara kwa mafanikio mbele ya ubeberu na mashinikizo ya kila upande ya Marekani na waitifaki wake, kumeipa uwezo Jamhuri ya Kiislamu wa kuamini kwamba, muqawama wa taifa lililoshikamana vilivyo na lenye nia ya kweli unaweza kushinda uadui na inadi zote za maadui na kujifungulia njia yenye fakhari kubwa kuelekea kwenye malengo yake makubwa. Maendeleo ya kila upande ya nchi yetu katika miongo miwili iliyopita ni uhakika ambao uko wazi mbele ya macho ya watu wote na vituo rasmi vya kimataifa vimekuwa vikilikiri jambo hilo mara kwa mara na kwamba mafanikio yote haya yamepatikana nchini Iran katika mazingira ya vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi na mashambulizi makubwa ya kipropaganda ya kanali zenye mfungamano na Marekani na Uzayuni. Vikwazo ambayo mabeberu wameviita ni vya kutia ulemavu si tu havitatutia ulemavu, bali vitazifanya hatua zetu ziwe makini zaidi, hima yetu iwe kubwa zaidi na kujiamini kwetu kuwe kukubwa zaidi kwa ajili ya kuchanganua mambo kwa njia sahihi zaidi na kwa ajili ya kutumia kwa njia bora zaidi uwezo wa ndani ya taifa letu. Sisi tumeshuhudia mara nyingi mno msaada wa Mwenyezi Mungu kwetu katika kukabiliana na changamoto hizi.
Wageni wapendwa!
Nahisi ni wajibu wangu hapa kuzungumzia suala jingine muhimu ingawa linahusiana na eneo letu hili lakini lina mambo mengi ambayo yanakwenda hadi nje ya masuala ya eneo hili na kuathiri siasa za kimataifa kwa miongo yote hii nalo ni suala lenye maumivu mengi la Palestina. Muhtasari wa kadhia hiyo ni kwamba nchi moja huru na inayojulikana vyema kihistoria inayojulikana kwa jina la Palestina - kutokana na njama za kutisha za Magharibi zikiongozwa na Uingereza - iliporwa kutoka mikononi mwa watu wake wa asili katika karne ya 40 kwa kutumia nguvu za silaha na mauaji na hila za kila namna na kukabidhiwa kwa kundi la watu ambao wengi wao walitoka katika nchi za Ulaya. Wizi na uporaji huo mkubwa ulianza kwa kuwaua kwa umati wananchi wasio na ulinzi katika miji na vijiji vya Palestina na kuwafukuza kutoka katika nyumba na makazi yao na kuwafanya wawe wakimbizi katika nchi jirani na hadi leo hii jinai hizo zingali zinaendelea. Hili ni moja ya masuala muhimu sana kwa jamii ya mwanadamu. Viongozi wa kisaisa na kijeshi wa utawala ghasibu wa Kizayuni katika kipindi chote hiki hakuna jinai waliyoacha kuitenda, kuanzia kuua watu, kuharibu nyumba na mashamba yao, kuwatia mbaroni, kuwatesa wanaume na wanawake na hata watoto wadogo; hadi kudhalilisha na kukashifu heshima ya taifa hilo na kufanya njama za kuliangamiza kabisa na kulitumbukiza taifa hilo kwenye tumbo linalokula haramu la utawala wa Kizayuni. Jinai hizo za Wazayuni pia zimefanyika kupitia kushambulia kambi za wakimbizi wa Palestina ndani ya Palestina kwenyewe na katika nchi jirani ambako kuna mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina. Majina ya "Sabra" na "Shatila" na "Qana" na "Dir Yasin" na mfano wake yameandikwa kwa damu ya wananchi madhlumu wa Palestina katika historia ya eneo hili. Hivi sasa pia na baada ya kupita miaka 65 bado jinai hizo za mbwa mwitu katili yaani utawala wa Kizayuni zinaendelea dhidi ya Wapalestina waliobakia katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu. Kila kukicha Wazayuni wanafanya jinai mpya mpya na kulitumbukiza eneo hili katika migogoro mipya mara kwa mara. Ni mara chache sana hutosikia habari za kuuliwa na kujeruhiwa na kutiwa mbaroni vijana wa Kipalestina ambao wamesimama imara kulinda na kutetea nchi yao na kupinga kuharibiwa nyumbani na mashamba yao. Kwa kuanzisha vita angamizi na vya mauaji makubwa ya watu, na kukalia kwa mabavu ardhi za Waarabu na kupanga ugaidi wa kiserikali katika eneo hili na duniani kwa ujumla; utawala wa Kizayuni umeanzisha makumi ya miaka ya mauaji ya kigaidi, vita na vitendo vingi vya kishari na viovu na kulizuia kupata haki zake taifa la Palestina lililosimama imara kupigania haki zake. Taifa hilo la Palestina limepachikwa jina la ugaidi na kanali za Kizayuni huku vyombo vingine vingi vya nchi za Magharibi na vibaraka wao vikiendelea kukanyaga maadili yao yote ya upashaji habari ili kueneza na kukariri uongo huo mkubwa. Viongozi wa kisiasa wanaodai kutetea haki za binaadamu nao wanauunga mkono utawala huo unaosababisha maafa makubwa bila ya kuona haya wala soni, bali viongozi hao wamekuwa kama mawakili wa kuutetea utawala huo.
Tunachosema sisi ni kuwa, Palestina ni mali ya Wapalestina wote na kuendelea kukaliwa kwa mabavu Palestina ni dhulma kubwa, ni kitu kisichovumilika na ndiyo hatari kubwa zaidi kwa usalama na amani ya dunia. Njia zote zilizopendekezwa na kufuatwa na Wamagharibi na waitifaki wao kwa ajili ya utatuzi wa kadhia ya Palestina ni ghalati na zimefeli na katika siku za usoni pia zitashindwa tu. Sisi tumependekeza njia ya kiadilifu na ya kidemokrasia kikamilifu kwa ajili ya kutatua kadhia hiyo nayo ni kuwa: Wapalestina wote wawe ni wale waliomo ndani ya ardhi za Paletina hivi sasa au waliofukuzwa nje ya ardhi hizo na ambao bado wanatambulika kuwa ni Wapalesina, wawe Waislamu, Wakristo au Mayahudi wote washirikishwe kwenye kura ya maoni itakayosimamiwa vizuri na kwa njia inayokubaliwa na wote ili kujiamulia wenyewe muundo wa kisiasa wa nchi yao na Wapalestina wote waliopata mateso makubwa kwa miaka mingi sasa waweze kurejea nchini mwao na kupitia kura hiyo ya maoni kuandaliwe katiba na uchaguzi utakaowashirikisha Wapalestina wote hao. Wakati huo ndipo amani itaweza kupatikana.
Hapa ninapenda kuwapa viongozi wa Marekani ushauri kwamba hadi sasa na siku zote hizi mumekuwa mkijitokeza kama waungaji mkono na watetezi wa utawala wa Kizayuni lakini mnapaswa kutambua kuwa hadi hivi sasa utawala huo umeshakusababishieni matatizo mengi, umekuharibieni yenu na kuyafanya mataifa ya eneo hili yakuchukieni na kukuoneni ni washirika wa jinai za Wazayuni maghasibu, serikali na wananchi wa Marekani wamepata hasara kubwa ya kimaada na kimaanawi katika kipindi hiki cha miaka mingi kutokana na jambo hilo, mumepata hasara kubwa kupindukia, na kuna uwezekano gharama mtakazobeba zikawa kubwa zaidi katika siku za usoni kama mtaendelea na njia hiyo hiyo. Njooni na muutie akilini ushauri wa Jamhuri ya Kiislamu wa kufanyika kura ya maoni huko Palestina ili muweze kutoka katika utata huu mkubwa usiotatuka. Bila ya shaka wananchi wa eneo hili na watu wote wenye fikra huru duniani wataipokea vizuri hatua yenu hiyo.
Wageni wapendwa!
Sasa narejea katika matamshi yangu ya awali. Hali inayoukabili ulimwengu hivi sasa ni nyeti, na dunia sasa hivi inapita katika kipindi muhimu mno cha historia. Kinachotarajiwa ni kuona kunazaliwa mfumo mpya duniani. Majimui ya nchi wanachama wa NAM inaunda takriban thuluthi mbili ya wanachama wa jamii ya kimataifa na inaweza kutoa mchango mkubwa katika muundo wa baadaye wa mfumo wa dunia. Kufanyika mkutano huu mkubwa hapa Tehran nako; pekee ni tukio lenye maana kubwa ambalo inabidi liingizwe katika mahesabu. Iwapo sisi wanachama wa harakati hii tutaweza kuongeza ushirikiano wetu katika kuzidisha uwezo na suhula zetu, tutaweza kutoa mchango mkubwa wa kihistoria na wa kuweza kudumu milele katika juhudi za kuiokoa dunia kutokana na ukosefu wa amani, vita na ubeberu.
Jambo hilo litawezekana tu kwa kuwepo ushirikiano wa pande zote baina yetu. Kati yetu; nchi zenye utajiri mkubwa sana na zenye ushawishi mkubwa kimataifa, si chache. Ni jambo linalowezekana kabisa kutatua matatizo yaliyopo kupitia kushirikiana kiuchumi, kihabari na kuzidi kubadilishana tajiriba na uzeofu wenye kujenga. Inabidi tutie nia za kweli; tuendelee kuwa waaminifu katika malengo yetu; tusitishwe na kununa na kufinga uso madola ya kibeberu na wala tusitiwe tamaa na tabasamu zao; tujue kuwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu na utengenezaji wa sheria nzuri ndiko kutakakotusaidia. Kufeli kambi ya kikomonisti miongo miwili iliyopita na kushindwa siasa zinazodaiwa za demokrasia ya kiliberali ya Magharibi hivi sasa tukufanye kuwa ni funzo na somo kwetu. Na hatimaye kuporomoka madikteta vibaraka wa Marekani na marafiki wa utawala wa Kizayuni huko kaskazini mwa Afrika, na kushamiri mwamko wa Kiislamu katika nchi za eneo hili tukuhesabu kuwa ni fursa kubwa kwetu. Sisi tunao uwezo wa kunyanyua uwezo wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM wa kustafidi vizuri na masuala ya kisiasa katika kusimamia na kuongoza masuala ya dunia. Tunaweza kuandaa sanadi ya kihistoria ya kuweza kuleta mabadiliko katika maongozi ya dunia na kuandaa pia njia za kutekeleza sanadi hiyo; tunaweza kubuni mpango mzuri wa kupiga hatua kuelekea kwenye ushirikiano wenye faida wa kiuchumi na kutoa kigezo kizuri cha mawasiliano ya kiutamaduni baina yetu. Bila ya shaka yoyote kama kutaundwa sekretarieti yenye nguvu na amilifu ya kufuatilia mambo hayo kutaweza kusaidia kufikiwa malengo hayo adhimu na yenye taathira kubwa.
Ahsanteni.
1088072
captcha