IQNA

Kitengo cha nakala za kale za Qur’ani tukufu katika Jumba la Makumbusho la Haram Takatifu ya Bibi Maasouma (SA) katika mji wa Qum nchini Iran lina aina mbali mbali za Qur’ani za kale ambazo zimeandikwa kwa kaligrafia zenye mvuto. Aidha katika maonyesho hayo kuna misahafu iliyoandikwa kwa wino wa dhahabu pamoja na mapambo mengine ya kipkee katika kurasa na pia katika jildi. Baadhi ya nakala za Qur’ani katika jumba hilo la makumbusho ni zilizoandikwa katika zama za awali za Uislamu yaani katika karne za pili na tatu Hijria wakati wa zama za utawala wa Makhalifa wa silsila ya Bani Abbas. Aidha kuna nakala za Qur’ani za zama watawala walioshika mamlaka Iran katika silsila ya za kifalme za Ale Buye, Seljuki, Ilhani, Taimuri, Safavi na Qajari.

Aghalabu ya nakala za Qur’ani katika jumba hilo la makumbusho ni za zama za utawala wa silsila ya watawala wa Safavi nchini Iran kwani katika kipindi hicho cha historia ya Iran kulishuhudiwa kilele cha kunawiris taaluma mbali mbali za sanaa ikiwa ni pamoja na upambaji vitabu.