Mayahudi wa mji Shiraz kusini mwa Iran katika Sinagogi la Rabizadeh walijiunga na Mayahudi wa miji tofauti kote nchini kulaani jinai za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi katika Ukanda wa Gaza.
Mayahudi wa Iran jana walikusanyika kwa wakati mmoja katika miji ya Tehran, Shiraz, Isfahan, Yazd, Kermanshah na Kurdistan na kutaka vita visimamishwe mara moja huko Gaza na Palestina kwa ujumla.
Kuhani (Rabbi) Yunus Hamami Lalezad, kiongozi wa kidini wa Mayahudi wa Iran amesema katika hadhara ya Mayahudi waliojumuika pamoja hapa mjini Tehran kupinga jinai za utawala wa Kizayuni kwamba, wafuasi wa dini tofauti wanaishi pamoja hapa nchini Iran; na licha ya propaganda nyingi ambazo zimefanywa baada ya Mapinduzi lakini Mayahudi wa hapa nchini wameendelea kuwa na masinagogi na mijumuiko yao na hawajawahi kubughudhiwa na kusumbuliwa kwa namna yoyote ile.
Kuhani Lalezad ameongeza kuwa, Imam Khomeini (MA) na Ayatullah Khamenei daima wamekuwa wakiwajali Wayahudi; na Wayahudi, Wazartoshti na Wakristo wanaishi kwa amani na utulivu nchini Iran.
Kiongozi huyo wa kidini wa Mayahudi nchini Iran amesisitiza kuwa, Mayahudi wako pamoja na watetezi wengine wa uhuru duniani kuwaunga mkono wananchi wa Palestina wanaodhulumiwa.
Mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni katika maeneo ya makazi ya Ukanda wa Gaza yanaendelea kwa wiki ya nne mfululizo, na kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, zaidi ya Wapalestina elfu nane wameuawa shahidi, nusu yao wakiwa ni watoto wadogo madhulumu na wasio na ulinzi.













































