Maadhimisho ya Arbaeen hufanyika siku ya 40 baada ya Ashura, ukumbusho adhimu wa kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) ambaye aliuawa shahdi na jeshi katili la la Yazid katika vita vya Karbala mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia.
Kila mwaka mamilioni ya Mashia na pia idadi kubwa ya wasiokuwa Mashia humiminika katika mji Karbala nchini Iraq, mji ulipo Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS) ili kushiriki katika shughuli za maombolezo. Wafanya ziara, hasa kutoka Iraq na Iran, husafiri mamia ya kilomita kwa miguu hadi mji mtakatifu wa Karbala. Arbaeen ya mwaka huu inatarajiwa kuanguka mnamo Agosti 25, kulingana na kuonekana kwa mwezi.