IQNA

Waziri Mkuu wa Uturuki na mawaziri wake kuhudhuria maombolezo ya Ashura

17:18 - December 05, 2010
Habari ID: 2042692
Racep Tayyib Erdogan Waziri Mkuu wa Uturuki akiongoza baraza lake la mawaziri anatazamiwa kushiriki katika maombolezo ya kuuawa shahidi Imam Hussein (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) na wafuasi wake waaminifu huko Karbala katika ardhi ya Iraq.
Maombolezo hayo yamepangwa kufanyika siku ya Ijumaa Disemba 16 katika mji wa Istanbul. Akizungumza hivi karibuni katika swala ya Ijumaa ya mjini Istanbul Selahattin Ozgunduz msimamizi wa Msikiti wa Zeinabiyye wa mji huo amesema kuwa mwaka huu maombolezo hayo ya kimataifa ya Ashura yatahudhuriwa na Waziri Mkuu wa Uturuki akiandamana na baraza lake la mawaziri pamoja na wabunge wa nchi hiyo. Maombolezo hayo yamepangwa kufanyika katika uwanja wa Helkali mjini Istanbul.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Ozgunduz amesema kuwa ofisi za waziri mkuu pamoja na meya wa mji huo tayari zimetuma barua rasmi zikithibitisha kwamba viongozi na maafisa waliotajwa watashiriki katika maombolezo hayo jambo ambalo amesema linatia moyo kwa kutilia maanani kwamba mara hii serikali na taifa la Uturuki watashirikiana katika kuhuisha maombolezo hayo ya mjukuu wa Mtume (saw).
Tunakumbusha hapa kuwa Jumuiya ya Elimu, Utafiti na Ustawi ya Ja'fari ya Uturuki, CAFERIDER huandaa maombolezo ya kimataifa ya Ashura ambayo huhudhuriwa na malaki ya watu. Maombolezo hayo yanachukuliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kuwa maombolezo yanayofanyika kwa utaratibu mzuri zaidi duniani. 705766
captcha