IQNA – Angalau wagombea saba Waislamu, seneta mmoja na wajumbe sita wa Baraza la Wawakilishi, wameshinda viti katika Bunge la Congress (Kongresi) katika uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika Jumanne, na kuandika ongezeko la kihistoria katika mabunge yote mawili.
Uchaguzi huo ulibadilisha mlingano wa madaraka mjini Washington, ambapo chama cha upinzani cha Democratic kilishinda udhibiti wa Seneti na Baraza la Wawakilishi kutoka kwa chama tawala cha cha Republican.
Baadhi ya wabunge wapya na wale waliochaguliwa tena walifanya kampeni kwa kutegemea matukio ya kimataifa, misaada ya kibinadamu, na upinzani dhidi ya msaada wa kijeshi usio na masharti wa Marekani kwa Israel wakati mauaji ya halaiki yanayoendelea Gaza.
Abdul El-Sayed, Michigan
Mgombea huyo wa Democratic mwenye umri wa miaka 42 alimshinda aliyekuwa Mwakilishi wa Republican, Mike Rogers, na kuwa Muislamu wa kwanza kuchaguliwa katika Seneti ya Marekani.
Daktari na aliyekuwa afisa wa afya ya umma, El-Sayed alishinda kiti kilichoachwa wazi na Seneta Gary Peters anayestaafu, kufuatia kampeni yenye mvutano mkubwa ambamo dini yake ilikuwa shabaha ya mashambulizi kutoka kwa Warepublican na Rais Trump.
El-Sayed, aliyeshinda uchaguzi wa mchujo wa Democratic mwezi Agosti, alikosoa uhamishaji usio na masharti wa silaha za Marekani kwa Israel, na akaeleza operesheni zake za kijeshi Gaza kuwa ni mauaji ya halaiki.
Aliyekuwa mpinzani wake katika mchujo, Mwakilishi Haley Stevens, alimuunga mkono Rogers siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu kutokana na kauli za El-Sayed.
Adam Hamawy, New Jersey
Mdemocrat huyo mwenye umri wa miaka 56 alimshinda Mrepublican Gregg Mele katika Jimbo la Bunge la 12 la jimbo hilo, na kuwa Muislamu wa kwanza kuchaguliwa kuliwakilisha New Jersey katika Congress.
Daktari wa upasuaji wa kurekebisha umbo, daktari mstaafu wa vita wa Jeshi la Marekani na mwanajeshi mkongwe wa Vita vya Iraq, Hamawy alijitolea katika Hospitali ya Ulaya huko Gaza mwaka 2024.
Alifanya kampeni ya kuwepo kwa mtibabu kwa wote, kufutwa kwa madeni ya matibabu na ya wanafunzi, kukomeshwa kwa kamatamata dhidi ya wahamiaji inayotekelezwa Idara ya Utekelezaji wa Sheria za Uhamiaji na Forodha (ICE), na kukomeshwa kwa msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Israel.
Darializa Avila Chevalier, New York
Mdemocrat huyo alipata kiti cha Baraza la Wawakilishi baada ya kumshinda hapo awali mbunge wa muda mrefu Adriano Espaillat katika uchaguzi wa mchujo wa Juni.
Chevalier, mchunguzi wa haki za kiraia, mwanafunzi wa shahada ya udaktari wa falsafa na mwenye kusilimu, alishinda zaidi ya asilimia 85 ya kura.
Kampeni yake ililenga uratibu wa jamii na kutetea haki za Wapalestina.
Wabunge Waislamu Waliopo Warejesha Viti Vyao
Wajumbe wanne Waislamu wa Baraza la Wawakilishi walishinda uchaguzi upya kwa muhula wa miaka miwili, na kuendeleza majukumu yao katika mijadala ya Congress kuhusu sera za kigeni na haki za Wapalestina.
Rashida Tlaib, Michigan
Mdemocrat huyo Mmarekani mwenye asili ya Palestina alipata muhula wa tano akiwakilisha Jimbo la Bunge la 12 la jimbo hilo, baada ya kumshinda Mrepublican James Hooper.
Akiwa Mmarekani pekee mwenye asili ya Palestina katika Congress, Tlaib ametetea utekelezaji wa kanuni za ndani na za kimataifa kuhusu silaha, ulinzi wa raia na haki ya Wapalestina ya kujiamulia mambo yao.
Ilhan Omar, Minnesota
Mdemocrat huyo alishinda muhula wa tano akiwakilisha Jimbo la Bunge la 5 la jimbo hilo, baada ya kuwashinda Mrepublican John Nagel na mgombea huru DeVelle Jackson.
Omar, aliyewasili Marekani akiwa na umri wa miaka 12, alikua mbunge wa kwanza wa shirikisho nchini humo mwenye asili ya Somalia alipoingia madarakani mwaka 2019.
Ametetea misaada ya kibinadamu na uangalizi wa uhamishaji wa silaha wa Marekani, huku akikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya kisiasa kuhusu asili yake.
Andre Carson, Indiana
Mdemocrat huyo alihifadhi kiti chake cha Jimbo la Bunge la 7 lenye makao yake Indianapolis dhidi ya Mrepublican Patrick McAuley na Mlibertarian James Sceniak.
Akihudumu tangu mwaka 2008, Carson ndiye mbunge Muislamu aliyehudumu muda mrefu zaidi katika Baraza la Wawakilishi.
Misimamo yake ya kisera imesisitiza taasisi za kisheria za kimataifa, utu sawa wa binadamu na misaada ya kibinadamu.
Lateefah Simon, California
Mdemocrat huyo alihifadhi kiti chake akiwakilisha Jimbo la Bunge la 12 la jimbo hilo katika East Bay, baada ya kumshinda Mdemocrat mwenzake Jamie Joyce.
Simon amepinga uwasilishaji wa silaha za mashambulizi wa Marekani.
Wakati huohuo, mgombea Muislamu Aisha Wahab alidumisha uongozi wa awali katika kinyang’anyiro kingine cha Congress huko California huku zoezi la kuhesabu kura likiendelea.
3499678