IQNA – Maafisa wanasema dhoruba imezamisha mahema 70,000 Gaza, na upungufu wa vifaa umewaacha waokoaji wakihangaika kuzisaidia familia zilizofurushwa makwao huku utawala dhalimu wa Israel ukiendeleza mauaji ya kimbari na mzingiro katika eneo hilo.
Familia za Wapalestina waliofurushwa makwao zimebaki bila makazi baada ya mvua kubwa na pepo kali kuyazamisha mahema 70,000 katika Ukanda wa Gaza, huku maafisa wakionya kwamba miundombinu iliyoharibiwa na upungufu wa vifaa vinaelemea juhudi za dharura.
Dhoruba hiyo, iliyoanza usiku wa Ijumaa, pia iliangusha kuta kadhaa, kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Serikali. Ofisi hiyo ilikadiria hasara ya awali kuwa takriban dola milioni 3.
Vyanzo vya kitabibu vilisema Wapalestina watano walijeruhiwa wakati kuta mbili za majengo yaliyoharibiwa na mashambulizi ya awali ya Israel zilipoanguka, na bati moja lilianguka wakati wa dhoruba.
Msemaji wa Manispaa ya Gaza, Hosni Muhanna, alisema familia ambazo mahema yao yaliharibiwa hazina mahali pa kukaa.
Alisema takriban wakazi na waliofurushwa milioni 1 wamesongamana katika asilimia 30 hivi ya eneo la Mji wa Gaza, jambo linaloongeza mzigo kwa miundombinu iliyoharibiwa vibaya na vita vya mauaji ya halaiki vya Israel.
Muhanna alisema mji huo ulipokea milimita 60 za mvua ndani ya saa 12, sawa na takriban asilimia 15 ya mvua yake ya mwaka mzima. Pepo kali zilipeperusha baadhi ya mahema na kuyararua mengine, huku maji ya mvua yakiingia na kuzamisha makazi hayo.
Vikosi vya manispaa vilipokea simu 250 zikiripoti mafuriko barabarani, mmomonyoko wa ardhi na mifereji iliyoziba. Vilishughulikia nyingi kati ya hizo kwa kutumia rasilimali chache zilizopo, alisema.
Muhanna alionya kwamba kambi na maeneo 270 ya hifadhi katika Mji wa Gaza yako hatarini kukumbwa na mafuriko. Uharibifu uliotokana na vita umepunguza uwezo wa mfumo wa mifereji ya maji hadi asilimia 20, na kuacha mitaa ya nyanda za chini ikiwa katika hatari zaidi.
Alitaka vivuko vifunguliwe kikamilifu ili vifaa vya msimu wa baridi, misaada na mitambo mizito viweze kuingia Gaza.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, lilisema Alhamisi kwamba watu milioni 1.98, takriban asilimia 94 ya wakazi wa Gaza, wanahitaji makazi na bidhaa nyingine muhimu, likitaja tafiti zilizofanywa mwezi Juni. Lilisema asilimia 58 wanakabiliwa na mahitaji makubwa au ya kutisha ya makazi.
/3499710