IQNA

Serikali ya Taliban, Afghanistan yataka nchi za Waislamu ziitambue

21:11 - January 19, 2022
Habari ID: 3474827
TEHRAN (IQNA)- Waziri Mkuu wa serikali ya Taliban nchini Afghanistan ametoa wito kwa nchi za Waislamu ziitambue rasmi serikali hiyo.

Hadi sasa hakuna nchi yoyote duniani iliyoitambua rasmi serikali ya Taliban nchini Afghanistan."Natoa wito kwa nchi za Waislamu ziongoze katika kututambua rasmi. Hilo likifanyika natumai tutaweza kustawi kwa kasi," amesema Waziri Mkuu Mohammad Hassan Akhund katika kikao na waandishi habari mjini Kabul ambacho kimeitishwa Jumatano kujadili matatizo makubwa ya kiuchumi nchini humo.

Amesema kutambuliwa rasmi serikali hiyo si kwa ajili ya kuwanufaisha viongozi bali ni kwa maslahi ya wananchi huku akisisitiza kuwa Taliban imechukua hatua zote zenye lengo la kurejesha amani na usalama Afghanistan. Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu wa Serikali ya Taliban Abdul Salam Hanafi amesisitiza kuwa pamoja na kuwa wanataka kutambulia rasmi, hilo halimaanishi kuwa Taliban iko tayari kutoa mhanga uhuru wa kiuchumi ili kuwaridhisha wafadhili.

Hivi karibuni, Umoja wa Mataifa na washirika wake ulizindua mpango wa kusaidia watu milioni 28 wenye uhitaji mkubwa wa misaada ya kubinadamu nchini Afghanistan pamoja na nchi nyingine jirani.

Umoja wa Mataifa na mashirika matano yasiyo ya kiserikali yamelenga kuwasaidia wananchi milioni 22 wa Afghanistan pamoja na wengine milioni 5.7 wanaoishi kama wakimbizi katika nchi tano jirani sambamba na jamii za wazawa zilizowakaribisha.

Majanga ya kibinadamu yanaendelea kuikabili nchi hiyo ambapo taarifa zinaeleza kuwa nusu ya watu wanakabiliwa na njaa kali, zaidi ya watu milioni 9 wamekimbia makazi yao, mamilioni ya watoto hawaendi shule, ukiukwaji wa haki za kimsingi za wanawake na wasichana, wakulima na wafugaji wanataabika huku kukiwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa, na uchumi unazidi kudorora. Na kama hayo hayatoshi makumi ya maelfu ya watoto wako katika hatari ya kufa kutokana na utapiamlo huku huduma za kimsingi za afya zikiporomoka.

3477449

captcha