IQNA

Rouhani asema OIC ina jukumu la kuzuia mauaji ya Waislamu duniani

10:57 - February 07, 2014
Habari ID: 1371831
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuzuia unyanyasaji na mauaji ya Waislamu duniani ndio jukumu kuu la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Rais Rouhani amesema hayo leo mjini Tehran katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa OIC Iyad Amin Madani na kuongeza kuwa kuimarisha uhusiano wa pande zote na nchi za Kiislamu hasa nchi jirani ndiyo kipaumbele katika sera za kigeni za serikali ya Iran. Rais Rouhani ameongeza kuwa Waislamu duniani wana matarajio makubwa kuhusu OIC na hivyo juhudi zinapaswa kufanyika ili kukidhi matarajio hayo. Dakta Rouhani pia ameashiria wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na misimamo mikali ambayo inawanufaisha maadui wa Uislamu na kutoa wito kwa OIC kukabiliana na njama hizo sambamba na kuwasilisha taswira sahihi ya Uislamu duniani. Rais wa Iran amesisitiza kuwa OIC inapaswa kuhakikisha kuwa sauti ya Waislamu duniani inasikika, matusi dhidi ya Uislamu yanakomeshwa na kufanyike juhudi kubwa za kuzikomboa ardhi za Palestina.
Kwa upande wake Madani amesisitiza juu ya nafasi muhimu ya Iran katika kutatua migogoro ya ulimwengu wa Kiislamu. Aidha ameishukuru Iran kwa mchango wake mkubwa kwa kazi za OIC.
Madani aliyewasili Tehran Jumanne pia amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif. Katika mazungumzo hayo Zarif amesisitiza kuwa Iran haiwezi kuacha haki yake ya kumiliki teknolojia ya nyuklia. Zarif aidha amesistiza juu ya nafasi muhimu ya OIC katika kutetea haki za Wapalestina.
Jumuiya ya Nchi za Kiislamu iliundwa mwaka 1969 kwa lengo la kuimarisha umoja baina ya nchi za Kiislamu katika kukabiliana na njama za maadui na kutekeleza kivitendo matakwa ya Waislamu. Miongoni mwa matukio yaliyopelekea kuundwa OIC yenye wanachama 57, ni kuchoma moto Masjidul Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu. Jumuiya hiyo ambayo mwaka 2011 ilibadilishwa jina na kuwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, imezidi kuzingatiwa na fikra za waliowengi katika ulimwengu wa Kiislamu.
1371295

captcha