IQNA

Hispania na Brazil zailaani Israel kwa kuwateka raia wao katika bahari ya kimataifa

15:35 - May 02, 2026
Habari ID: 3482192
IQNA – Utawala wa Israel unakabiliwa na ukosoaji wa pamoja usio wa kawaida kutoka Hispania na Brazil baada ya jeshi lake la wanamaji kuwakamata raia wawili wa nchi hizo kutoka katika meli iliyokuwa ikielekea Gaza katika maji ya kimataifa, kitendo ambacho serikali zote mbili zimesema ni kinyume cha wazi cha sheria za kimataifa.

Katika taarifa ya pamoja, serikali za Hispania na Brazili zilisema wanaharakati hao wawili walikuwa ndani ya meli za msafara wa Sumud, ambao ulizuiwa na vikosi vya Israel katika maji ya kimataifa, na hawakuachiliwa “wakati meli zilipokamatwa wala baada ya kushushwa kwa abiria na wafanyakazi katika kisiwa cha Krete.”

“Kitendo hiki ni kinyume cha sheria za kimataifa na Israel inaweza kufikishwa mbele ya mahakama za kimataifa. Aidha kitendo hicho cha Israel kinaweza kuwa kosa la jinai chini ya sheria za kitaifa za Brazil na Uhispania,” ilionya taarifa hiyo.

Serikali za Hispania na Brazili zimeutaka utawala wa Israel urejeshe mara moja raia wao kwa dhamana kamili ya usalama, na kuruhusu upatikanaji wa haraka wa huduma za kibalozi kwa ajili ya msaada na ulinzi wao.

Msafara wa misaada ya kibinadamu wa kimataifa wa Sumud ulishambuliwa Alhamisi karibu na kisiwa cha Ugiriki, umbali wa takriban maili 600 za baharini kutoka eneo ambalo ulikusudia kufika yaani Ukanda wa Gaza unaokumbwa na mzingiro mkali.

Meli za kwanza za msafara huo, zilizokuwa zimebeba misaada ya kibinadamu, ziliondoka Barcelona tarehe 12 Aprili, huku msafara mkuu ukiondoka katika kisiwa cha Sicilia nchini Italia tarehe 26 Aprili, ukiwa na lengo la kuvunja mzingiro wa muda mrefu uliowekwa na Israel dhidi ya Gaza.

Israel imeweka mzingiro mkali dhidi ya Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2007, hali iliyowaacha wakazi milioni 2.4 wa eneo hilo wakikabiliwa na hatari ya njaa.

Aidha Jeshi katili la Israel lilianzisha mashambulizi makali ya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mwezi Oktoba 2023, yaliyodumu kwa miaka miwili, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 72,000, majeruhi zaidi ya 172,000, pamoja na uharibifu mkubwa katika eneo hilo.

3497304

captcha