
Siku ya Alhamisi, waandaaji wa msafara wa meli za kibinadamu wa Global Sumud Flotilla walisema kuwa meli zao zilihujumiwa na vikosi vya Israel walipokuwa wakisafiri katika Bahari ya Mediterania.
Katika taarifa yao walisema:
“Boti zetu zilizingirwa na boti za kijeshi za kasi zilizojitambulisha kuwa za ‘Israel’, zikiwalenga washiriki kwa miale ya leza na silaha za nusu-otomatiki, huku zikiamuru watu waliokuwamo melini kwenda mbele ya boti na kupiga magoti.”
Kupitia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, kundi hilo liliongeza:
“Boti za kijeshi za Israel zimezingira msafara huu kinyume cha sheria katika maji ya kimataifa na kutishia utekaji pamoja na matumizi ya nguvu.”
Msafara huo pia uliripoti kupoteza mawasiliano na baadhi ya meli.
“Tumeacha kuwasiliana na meli 11, na vyombo vya habari vya Israel vinadai kuwa meli 7 zimekamatwa. Serikali za dunia zinapaswa kuchukua hatua mara moja kuilinda misafara hii.”
Redio ya jeshi la Israel, ikinukuu chanzo kisichotajwa jina, ilisema vikosi vya Israel vimeanza kuchukua udhibiti wa baadhi ya meli zilizokuwa zikielekea Gaza, huku meli saba kati ya meli 58 zikidaiwa kuzuiwa karibu na kisiwa cha Krete nchini Ugiriki.
Balozi wa utawala haramu wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon, alisema msafara huo “umesimamishwa kabla ya kufika” katika eneo aliloliita “eneo letu”, na kuwataja washiriki kuwa “kundi la watu wanaotafuta umaarufu.”
Kwa upande wake, Gur Tsabar, msemaji wa msafara huo, alieleza tukio hilo kuwa:
“Shambulio la wazi dhidi ya boti za kiraia zisizo na silaha katika maji ya kimataifa.”
Akizungumza na mtandao wa Al Jazeera kutoka Toronto, alisema operesheni hiyo inafanyika mamia ya maili kutoka Israel, huku meli zikizingirwa na kutishiwa kwa silaha.
“Hili ni kinyume cha sheria za kimataifa. Israel haina mamlaka katika maji haya. Kupanda meli hizi kwa nguvu ni kizuizi kisicho halali, ambacho kinaweza kufanana na utekaji katika bahari ya wazi,” alisema Tsabar.
Aliongeza:
“Ni muhimu serikali zote zichukue hatua sasa. Kila serikali ina wajibu wa kuwalinda zaidi ya raia 400 walioko katika meli hizi na kusimamia sheria za kimataifa. Kimya katika wakati huu ni ushiriki wa moja kwa moja katika dhuluma.”
Mwanaharakati Tariq Ra’ouf, aliyekuwa kwenye mojawapo ya meli hizo, alisema vikosi vya majini vya Israel vilizingira msafara huo kwa kutumia meli kubwa za kijeshi na boti ndogo za kasi.
“Kutoka kwenye meli hizo za kijeshi, boti ndogo za kijeshi zilianza kuzunguka meli zetu nyingi. Ndege zisizokuwa na rubani zimekuwa zikizunguka juu yetu na kutuangazia taa, na tumekuwa tukipokea ujumbe kupitia redio kutoka jeshi la Israel wakidai tunakiuka sheria za kimataifa na kwamba tunapaswa kusimama,” alisema.
Ra’ouf alieleza kuwa operesheni hiyo iliendelea kwa saa kadhaa, wakati msafara huo ulikuwa ukielekea kisiwa cha Krete katika maji ya kimataifa.
“Tayari tumepoteza mawasiliano na meli nyingi,” alisema, akiongeza kuwa mawasiliano ya msafara huo yalivurugwa kwa makusudi, huku jeshi la Israel likicheza muziki kupitia redio za mawasiliano kama mbinu ya vita vya kisaikolojia.
“Tunapatikana katika maji ya kimataifa, hivyo hili ni tukio lisilo la kawaida sana, kwa sababu hatuko hata karibu na Gaza,” aliongeza.
Vyanzo vya Israel vimedokeza kuwa operesheni hiyo ililenga kuuvuruga msafara huo kwa kuuzuia mbali na Gaza.
Wakati huo, meli hizo zilikuwa umbali wa takriban maili 600 za baharini (takriban kilomita 1,111) kutoka Gaza.
Katika matukio ya awali, vikosi vya Israel vilikuwa vikizuia misafara hiyo karibu zaidi na Gaza, huku tukio la mbali zaidi lililoripotiwa hapo awali likiwa umbali wa maili 72 za baharini (km 133).
Zaidi ya meli 50 zilizobeba wanaharakati kutoka nchi mbalimbali zilikuwa zimeondoka Italia siku chache zilizopita, katika kile ambacho waandaaji walikitaja kuwa jaribio kubwa zaidi la kupeleka msaada wa kibinadamu Gaza kupitia bahari. Eneo la Gaza limekuwa likikabiliwa na mauaji ya kimbari yanayotelezwa na utawala haramu wa Isarel tangu Oktoba 2023 mbali na mzingiro unaozuia chakula, dawa na mahitaji mengine kufika eneo hilo
Operesheni nyingine ya meli za misaada mnamo Oktoba mwaka uliopita ilishuhudia vikosi vya Israel vikizuia takriban meli 40 za msafara, na kuwakamata zaidi ya washiriki 450.
Miongoni mwa waliokamatwa wakati huo walikuwa mjukuu wa Nelson Mandela, mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg, na mbunge wa Bunge la Ulaya Rima Hassan.
Baadhi ya waliokamatwa baadaye waliripoti unyanyasaji wa kimwili na kisaikolojia wakiwa kizuizini, kabla ya utawala huo kuwafukuza kutoka nchini.
3497290