IQNA

Kiongozi Muadhamu atangaza 'Mwanzo Mpya' katika Mlango wa Bahari wa Hormuz

18:28 - May 01, 2026
Habari ID: 3482185
IQNA-Ayatullah Seyyed Mojtaba Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametangaza mwanzo wa “sura mpya” kwa Mlango Bahari wa Hormuz, njia ya kimkakati ya baharini.

Aidha amesisitiza kuwa Iran itaweka kanuni mpya za usimamizi katika Mlango wa Bahari wa Hormuz kufuatia uchokozi wa hivi karibuni wa Marekani na Israel dhidi ya nchi hiyo.

Ayatullah Khamenei alitoa kauli hizo katika ujumbe uliotolewa Alhamisi kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Ghuba ya Uajemi. Kila mwaka tarehe 30 Aprili, Iran hukumbuka ushindi wake wa kihistoria wa mwaka 1622 dhidi ya utawala wa kikoloni uliokuwa umeikalia kwa mabavu sehemu ya pwani yake ya kusini.

Maadhimisho ya mwaka huu yamekuja hasa miezi miwili tangu Marekani na utawala wa Israel walipoanzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran tarehe 28 Februari.

Katika ujumbe wake, Ayatullah Khamenei ameitaja Ghuba ya Uajemi kuwa ni “neema isiyoweza kubadilishwa” kwa mataifa ya Kiislamu ya eneo hilo. Amesema kuwa bahari hiyo pamoja na Mlango Bahari wa Hormuz “imeunda sehemu ya utambulisho na ustaarabu wetu, na zaidi ya kuwa kiungo kinachowaunganisha watu na mataifa, pia ni njia muhimu na ya kipekee kwa uchumi wa dunia.”

Aidha ameongeza kuwa, “Rasilimali hii ya kimkakati imechochea tamaa na uchu wa nguvu za kishetani katika karne nyingi zilizopita. Historia ya mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa madola ajinabi ya Ulaya na Marekani, hali ya ukosefu wa usalama, uharibifu, pamoja na vitisho vingi dhidi ya nchi za eneo hili, ni sehemu ndogo tu ya njama zenye madhara ambazo madola yenye kiburi duniani yamekuwa yakipanga dhidi ya wakazi wa eneo la Ghuba ya Uajemi. Mfano wa karibuni kabisa wa mienendo hiyo ni uhalifu wa hivi majuzi wa yule Shetani Mkuu.” Kiongozi Muadhamuh apo alikuwa akiashiria mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yaliyoanza tarehe 28 Februari.

Akiendelea, alisema kwamba kutokana na Iran kuwa na ufuo mrefu zaidi wa ardhi unaopakana na Ghuba ya Uajemi, taifa la Iran “limebeba mzigo mkubwa zaidi wa kujitolea kwa ajili ya uhuru wa Ghuba ya Uajemi na katika kukabiliana na ajinabi na wavamizi; kuanzia kuwaondoa Wareno na kukomboa Mlango wa Bahari wa Hormuz, hadi mapambano dhidi ya ukoloni wa Uholanzi na hamasa za mapambano dhidi ya ukoloni wa Uingereza, na kadhalika.”

Amesisitiza kuwa Mapinduzi ya Kiislamu yamekuwa “nukta muhimua katika mfululizo huo wa muqawama mapambano hayo, kwa kukata mikono ya madola yenye kiburi kutoka katika eneo la Ghuba ya Uajemi.”

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: “Leo, miezi miwili baada ya operesheni kubwa zaidi ya kijeshi na uchokozi uliofanywa na wababe wa dunia katika eneo hili, na kufuatia kushindwa kwa fedheha kwa Marekani katika njama yake, ukurasa mpya wa Ghuba ya Uajemi na Mlango wa Bahari wa Hormuz umeaanza kufunguka."

Kiongozi Muadhamu amebainisha kwamba mataifa ya eneo la Ghuba ya Uajemi yameshuhudia “umakini na ulinzi makini” wa vikosi vya wanamaji vya Iran katika kipindi cha siku sitini zilizopita.

Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: “Watu wa mataifa ya Ghuba ya Uajemi, ambao kwa miaka mingi walikuwa wamezoea ukimya na unyenyekevu wa watawala wao mbele ya wababe na wavamizi, wamejionea kwa macho yao wenyewe katika siku sitini zilizopita vielelezo vya kuvutia vya uimara, umakini na juhudi za wanaume jasiri wa vikosi vya wanamaji vya Jeshi la Iran na Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), sambamba na ari na ushujaa wa wananchi na vijana wa maeneo ya kusini mwa Iran, katika kukataa utawala wa kigeni."

Aidha amesema kuwa kufuatia vita vya hivi karibuni vilivyolazimishwa dhidi ya Iran, “imeonekana wazi si tu mbele ya maoni ya umma duniani na mataifa ya eneo hili, bali hata kwa watawala wa nchi mbalimbali, kwamba uwepo wa wageni kutoka Marekani na kujikita kwao katika ardhi za eneo la Ghuba ya Uajemi ndicho chanzo kikuu cha hali ya kukosekana kwa usalama katika eneo hili.”

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kwamba “kambi za Marekani zisizo na msingi thabiti hazina hata uwezo wa kujilinda zenyewe, sembuse kuwa na matumaini kwamba Marekani inaweza kulinda washirika wake wa eneo hili.”

Amebainisha kwamba mustakabali wa Ghuba ya Uajemi utakuwa “wenye mwanga” kwa kusema:

“Mustakabali wenye nuru wa eneo la Ghuba ya Uajemi utakuwa mustakabali usio na Marekani, na utakaohudumia maendeleo, ustawi na faraja ya mataifa yake.” Halikadhalika ameongeza kuwa Iran ina “hatima ya pamoja” na majirani zake wa Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.

Hata hivyo, ameongeza kuwa, “Wageni ambao kutoka maelfu ya kilomita mbali huja kwa tamaa na kufanya vitendo vya uonevu ndani ya eneo hili hawana nafasi humo isipokuwa chini ya kina cha maji yake.”

“Msururu wa ushindi huu,” aliendelea kusema, “ambao kwa neema ya Mwenyezi Mungu umefikiwa chini ya kivuli cha hatua na sera za muqawama pamoja na mkakati wa Iran iliyo imara, utakuwa mstari wa mbele katika kuibuka kwa mpangilio mpya wa kikanda na wa kimataifa.”

Aidha aliongeza kuwa, “Leo hii, mwamko wa kimiujiza wa taifa la Iran hauishii kwa makumi ya mamilioni ya watu walio tayari kujitoa mhanga katika mapambano dhidi ya Uzayuni na Marekani inayotuhumiwa kwa umwagaji damu.”

“Bali, wakiwa mstari wa mbele wa safu zilizoungana za Ummah wa Kiislamu uliopo katika mwamko mpya, raia wa Iran milioni tisini, wenye hamasa na heshima, walio ndani na nje ya nchi, wanachukulia utambulisho wao wote, uwezo wao wa kiroho, kibinadamu, kisayansi, viwandani, pamoja na rasilimali zao zote za kiteknolojia za msingi na za kisasa, kuanzia nano na bio hadi nyuklia na makombora, kama mali yao ya kitaifa, na watazilinda kama wanavyolinda mipaka yao ya baharini, ardhini na angani,” aliandika.

Ayatullah Khamenei alisisitiza kuwa, “Iran ya Kiislamu, kwa kuonyesha shukrani ya vitendo kwa neema ya kupewa jukumu la kusimamia Mlango wa Bahari wa Hormuz, itahakikisha usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi na kutokomeza matumizi mabaya ya njia hii ya bahari yanayofanywa na maadui wenye uhasama,” akibainisha kwamba njia hiyo ya kimkakati sasa itasimamiwa kwa mujibu wa kanuni mpya.

Ameongeza kuwa: “Kanuni za kisheria na utekelezaji wa usimamizi mpya wa Mlango wa Bahari wa Hormuz zitaleta faraja na maendeleo kwa manufaa ya mataifa yote ya eneo hili, na baraka zake za kiuchumi zitafurahisha mioyo ya wananchi; kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, hataka kama wasioamini watachukia."

3497292/

captcha