IQNA

Ujumbe wa Ghadir: Kuendelezwa suna za Mtume na kusimamishwa jamii ya Imam Ali

9:48 - December 16, 2008
Habari ID: 1719662
Hivi sasa tumo katika kipindi cha kuadhimisha sikukuu ya Ghadir Khum, siku ambayo kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika ndiyo “Idi kubwa zaidi ya Mwenyezi Mungu”. Ni siku ya kukamilishwa dini na neema ya Mola Mlezi.
Hata hiyo swali linaloulizwa hapa ni kuwa, ni nini siri ya adhama na utukufu wa siku ya Ghadir mbele ya Mwenyezi Mungu?
Je, hadi sasa tumejiuliza, ni nini majukumu yetu ya mtu binafsi na jamii kuhusu siku ya Ghadir?
Je, siri ya adhama ya siku hiyo ni kusherehekea tu na kuwafurahisha watu kwa kufanya mahfali na vikao vya sherehe?
Ni nini ujumbe wa siku ya Ghadir Khum kwa jamii ya Kiislamu ya mwanadamu wa leo na vizazi vijavyo?
Mwenyezi Mungu (saw) anasema katika suratul Maidah kwamba: Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako; na kama hutafanya, basi hukufikisha ujumbe wake. Hakika Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. (Maidah-67)
Je, hii leo ni nani mwenye jukumu la kufikisha na kutangaza ujumbe uliojaa hikima wa Ghadir katika ulimwengu wa Kiislamu, ambao ni ujumbe wa Uimamu na wilaya ya Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw)?
Kimsingi, Ghadiri ni nini? Nini siri ya adhama ya siku hiyo?
Falsafa ya Ghadir ni ile ile falsafa na kubaathiwa Mtume (saw) katika pango la Hiraa, au kwa maana nyingine ni Uimamu wa watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume na kuendeleza kazi na majukumu ya Nabii wa Mwenyezi Mungu (sw).
Mwenyezi Mungu (sw) ameiita siku ya Ghadir kuwa ni siku ya kukamilishwa dini, kwa hivyo ujumbe wa Ghadir ni harakati ya kila mtu katika jamii kuelekea kwenye ufanisi na ukamilifu na kujitenga na nakisi na upotovu.
Ghadir ni wenzo wa kupima ukweli na usahihi wa mifumo na madhehebu mbalimbali na dalili ya usafi wa sira ya wanadamu wote. Hii ni kwa sababu Ali bin Abi Twalib (as) ambaye ndiye muhusika mkuu wa siku hii ya Ghadir, ameitwa kwamba ni “Mizani ya matendo”.
Siku ya Ghadir inabeba ujumbe wa harakati halisi ya tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kusalimu amri mbele ya matakwa ya Allah (sw). Kwani ni Yeye Mwenyezi Mungu ambaye alisema katika siku hiyo ya Ghadir kwamba: “Na nimekuridhieni Uislamu kuwa dini”. Hivyo basi, harakati ya aina yoyote au maneno na mwenendo unaokwenda kinyume na ridhaa ya Mola Muumba huwa mbali na mafundisho ya Ghadir.
Ghadir ni kuukabidhi moyo na irada yako kwa mbora wa viumbe Muhammad (saw), na kwa msingi huo aina yoyote ya kukengeuka suna na mwenendo wa Mtume Muhammad huwa ni kujitenga na falsafa ya Ghadir.
Ghadir ni siku ya kuarifishwa kwa mara ya mwisho njia halisi ya uongofu na kiongozi wa njia hiyo.
Ghadir ni mwanzo wa wanadamu kuelekea kwenye thamani za kiroho za shakhsia asiyekuwa na kifani baada ya Mtume, yaani Ali bin Abi Twalib, ambaye alikuwa chemchemi ya mema, kigezo cha ukamilifu wa mwanadamu na uchamungu, dhihirisho la uadilifu, ikhlasi, upendo, ushujaa, amani, upole kwa watu wa jamii na mapambano dhidi ya upotofu na dhulma. Hivyo basi, kuwa mbali na shakhsia huyo kwa hakika ni kujitenga na saada, ufanisi na ukamilifu wa jamii ya Kiislamu na ubinadamu.
Ghadir ilikuwa bishara ya ujenzi wa jamii ya Imam Ali kwa msingi wa tauhidi, Utume wa Nabii Muhammad (saw), uadilifu, umoja na amani na kupambana na dhulma na uonevu.
Ghadir ni siku ya kuwakumbusha wanadamu majukumu yao na natija yake ni kutozembea katika kutekeleza amri za Mola Mlezi. Kwani katika siku hiyo Muhammad Mwaminifu (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake) alisema: Enyi watu! Hakika sijazembea katika kufikisha kwenu yale yaliyoteremshwa kwangu mimi. Hakika Malaika Jibril ameniletea ujumbe kutoka mwa Mola wangu akiniamuru kusimama hapa na kuwatangazia watu wote kwamba: “Ali bin Abi Twalib ni ndugu yangu, wasii wangu, khalifa wangu katika umma na Imamu baada yangu mimi. Yeye kwangu mimi ni kama Haruna kwa Musa, lakini hakuna Nabii baada yangu. Ali ndiye mwenye mamlaka juu yenu baada ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.”
Siku ya Ghadir Khum inabeba ujumbe wa umoja na udugu kati ya wafuasi wote wa Nabii Muhammad na mapambano dhidi ya mtengano na mfarakano. Kwa hivyo, aina yoyote ya mfarakano na hitilafu kati ya ndugu Waislamu na jamii za Kiislamu ni kinyume na falsafa ya Ghadir.
Kigezo kamili na bora zaidi cha warithi wa Ghadir ni sira na mwenendo wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Japokuwa alitangazwa na Mtume Muhammad (saw) katika siku ya Ghadir Khum mbele ya maelfu ya Waislamu kwamba ndiye Imamu na khalifa baada yake, lakini mtukufu huyo alipotambua kwamba kudai haki hiyo baada ya Mtume kurejea kwa Mola wake yumkini kukasababisha madhara kwa Uislamu wenyewe na kuzusha hitilafu, alifumbia macho haki yake na akatoa ushirikiano kwa wale waliochukua nafasi yake na kutawala jamii ya Kiislamu. Hii ni kwa sababu Uislamu unahitajia umoja na mshikamano, na kwa sababu hiyo Amirul Muuminin Ali (as) alijitolea muhanga katika kadhia hiyo. Naam, umoja na mshikamano wa Kiislamu ndiyo lengo kuu la Uimamu wa Ahlubait wa Mtume (saw).
Warithi wote wa Ghadir wanapaswa kufuata nyayo za Amirul Muuminin, baba wa umoja wa Kiislamu, kwa kufuata mafundisho ya Ahlubait wa Mtume na kubeba bendera ya kuwalingania umoja na mshikamano wafuasi wa madhehebu zote za Kiislamu.
Ewe Mola Mlezi! Shuhudia kwamba katika siku hii ya kuadhimisha mwaka wa 1419 wa tukio la Ghadir tunakariri yote aliyosema Mtume wako Mtukufu na kushikamana na dini aliyotuletea. Tunawapenda na kujikurubisha kwa wale aliowapenda. Tunaridhia na kuwafuata wale aliowaridhia yeye na kujitenga na kuwachukia wale aliowachukia yeye.

captcha