
Kupitia chapisho kwenye jukwaa la X, ofisi hiyo ilitoa wito wa hatua za haraka zaidi ya kulaani kwa maneno, ikitaka uwajibikaji, ulinzi wa wanahabari, na upatikanaji huru wa vyombo vya habari katika ukanda huo uliowekewa mzingiro.
Ofisi hiyo imesema: “Gaza ndiyo mahali hatari zaidi duniani kwa wanahabari.”
Taarifa hiyo imethibitisha vifo vya wanahabari 295 katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, idadi ya kutisha inayodhihirisha kwa uzito kile kinachoonekana kama kulengwa kwa kimfumo kwa wataalamu wa habari.
Chombo hicho cha Umoja wa Mataifa pia kimeangazia janga pana la kibinadamu, kikisema kuwa tangu Oktoba 7, 2023, vita vinavyoendelea vya Israel dhidi ya Gaza vimesababisha makumi ya maelfu ya Wapalestina kuuawa na kujeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Waathiriwa wengi bado wamekwama chini ya vifusi.
Taarifa hiyo imetolewa sambamba na maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambapo Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, alielezea vita hivyo kama “mtego wa mauti kwa vyombo vya habari.”
Makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakishutumu mara kwa mara Israel kwa kuwalenga kwa makusudi wanahabari na familia zao, pamoja na ofisi za vyombo vya habari, kwa lengo la kuzima ufunikaji wa taarifa kuhusu jinai zake Ukanda wa Gaza.
Utawala wa Israel haujaruhusu vyombo vya habari vya kigeni kuingia katika ukanda huo, ukidhibiti mtiririko wa taarifa na mara kwa mara kuzuia kazi za wanahabari wa Kipalestina.
Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imehimiza jumuiya ya kimataifa kuacha hatua za kulaani kwa maneno pekee na badala yake kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha uwajibikaji kwa mauaji hayo, kuwalinda wanahabari dhidi ya madhara zaidi, na kuruhusu vyombo vya habari kupata ufikiaji usio na vikwazo ili kurekodi jinao zinazotekelezwa dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
3497329