
Wizara ya Awqaf ya Misri siku ya Jumamosi iliadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Sheikh Muhammad Abdulaziz Hissan, mmoja wa nguzo muhimu katika qiraa au usomaji wa Qur’ani nchini Misri na katika ulimwengu wa Kiislamu.
Alizaliwa tarehe 22 Agosti 1928 katika kijiji cha Farstaq, mji wa Kfar Al‑Zayat, mkoa wa Gharbia nchini Misri, na alifariki dunia tarehe 2 Mei 2003.
Sheikh Hissan aliacha urithi mkubwa wa qiraa ya Qur’ani iliojaa unyenyekevu wa usomaji na shule mashuhuri ya sauti. Alikulia katika mazingira ya Qur’ani na akaweza kuihifadhi kikamilifu akiwa bado mtoto. Alipoteza uwezo wa kuonakatika utoto wake, jambo lililomfanya ajielekeze kikamilifu katika kuhifadhi Qur’ani kwa utulivu wa moyo na akili.
Muhammad Abdulaziz Hissan aliihifadhi Qur’ani kwa muda mfupi sana, kabla hajafikisha umri wa miaka saba, na akajifunza qira’aat saba za Qur’ani. Pia aliihifadhi Shatibiyyah (kitabu mashuhuri cha qira’a na tajwidi) ndani ya miaka miwili tu, hadi akawa miongoni mwa wanazuoni wa kanuni za tajwidi na usomaji.
Alifaidika sana na uwepo wa wanazuoni kadhaa, na kipaji chake katika sawt (sauti) kilianza kudhihirika mapema. Wapenzi wa Qur’ani walimpa majina mengi ya heshima, miongoni mwao “Qari Faqih” (qari mwenye hekima) na “Qari Nasr” (qari wa ushindi).
Qari huyu alikuwa bingwa katika waqf na ibtida’, sauti na maqam, na usomaji wake ulikuwa sahihi katika kufikisha na kufafanua maana za Qur’ani kwa namna ya kuvutia, yenye kugusa nyoyo, na ya kipekee kabisa.
Mnamo mwaka 1964, baada ya kufaulu mtihani wa Kamati ya Maqari, alijiunga na Redio ya Misri, ambako sauti yake ikawa miongoni mwa sauti mashuhuri katika usomaji wa redio, hususan katika usomaji wa Qur’ani wa asubuhi na Swala ya Ijumaa, na ikapokelewa kwa mapana ndani na nje ya Misri.
Sheikh Hissan alishiriki katika kufufua halaqa za Qur’ani ndani na nje ya Misri, hasa katika nchi za Ghuba ya Uajemi, na alipokea tuzo nyingi pamoja na barua za pongezi, ikiwemo barua ya heshima kutoka kwa Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan.
Qari huyu marehemu alikuwa na mtindo wa kipekee wa sauti na maqam, na aliacha mamia ya rekodi za usomaji ambazo bado zinasikilizwa hadi leo na wapenda Qur’ani, kama ushahidi wa kipaji chake kikubwa katika kusoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Siku moja, Sheikh Mahmoud Khalil Al‑Husari, qari mwingine mashuhuri wa Misri, alimwambia Hissan:
“Ewe Sheikh Muhammad! Una mustakabali mkubwa; kwa unyenyekevu wako na uwezo wako wa kuhuisha taswira za maana za Qur’ani, unanitetemesha moyoni, na sauti yako huigusa mioyo moja kwa moja.”
Sheikh Hissan aliteuliwa kuwa qari wa Msikiti wa Ahmadiy mjini Tanta mwaka 1980 kwa agizo la rais wa wakati huo wa Misri, Anwar Sadat. Alikuwa pia qari pekee katika historia ya redio na televisheni ya Misri aliyesoma Qur’ani ya asubuhi na ya Ijumaa katika miji miwili tofauti kupitia Redio ya Misri mwaka 1985.
Wizara ya Awqaf ya Misri, ikikumbuka kumbukumbu ya kifo cha qari huyu, ilisisitiza kuwa maadhimisho haya yanafanywa ili kuhifadhi na kuenzi safari ya maisha ya mmoja wa watu waliolitumikia Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa kufundisha, kusoma, na kwa mwenendo mwema. Katika taarifa yake ilisema:
“Tunaomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amrehemu kwa rehema nyingi na ajumuishe aliyoyafanya katika mizani ya mema yake.”
Katika jioni ya siku aliyofariki Sheikh Hissan, mke wake naye pia alifariki dunia, na wote wawili wakahamia Akhera siku moja. Aliacha urithi mkubwa wa zaidi ya saa 10,000 za usomaji wa Qur’ani kwa Redio ya Misri.
Allah amrehemu kwa rehema zake pana, na awajalie daraja za juu katika Pepo. Amina.
3497345