IQNA

Bunge la Kuwait lakosoa ugawaji wa nakala za Qur'ani zenye makosa ya kimaandishi

13:03 - December 18, 2008
Habari ID: 1720164
Wabunge wa Kuwait wamekosoa hatua ya Wizara ya Waqfu ya nchi hiyo ya kugawa nakala za Qur'ani zilizojaa makosa ya uchapishaji.
Mbunge Muhammad Hayif al Matiri ameeleza kustaajabishwa na uchapishwaji wa mara kwa mara wa nakala zenye makosa ya chapa za Qur'ani Tukufu na ameitaka Wizara ya Waqfu ya nchi hiyo kuunda tume maalumu ya kuchunguza suala hilo na kuzuia kukaririwa makosa hayo.
Al matiri amesema: Suala la uchapishwaji wa nakala zenye makosa ya kimaandishi nchini Kuwait limefikia kiwango ambacho hakiwezi kunyamaziwa kimya. Amesema, bunge la nchi hiyo litafuatilia kadhia hiyo ili kuwatambua wahusika ambao wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mbunge Askar al Anazi wa Kuwait pia amelaani uzembe wa Wizara ya Waqfu ya nchi hiyo na kutosimamia vyema kiwanda cha uchapishaji Qur'ani cha Kuwait huko Sudan ambacho kimechapisha nakala nyingi zenye makosa ya kimaandishi za Qur'ani. Al Anazi amesema: Watu waliohusika na kitendo hicho wanapaswa kufikishwa mahakamani. Amesisitiza juu ya udharura wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kuzuia kuchapishwa tena nakala zenye makosa ya kimaandishi za Qur'ani Tukufu ili kulinda utukufu wa kitabu hicho.
Mwaka 1999 bunge la Kuwait lilimwita na kumsaili Waziri wa Waqfu wa nchi hiyo kwa makosa ya kuzembea na kutofuatilia ipasavyo uchapishaji wa mara kwa mara wa nakala zenye makosa ya kimaandishi za Qur'ani Tukufu. 334617

captcha