IQNA

Kuanzishwa rasmi kitengo cha Kiswahili cha Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa IQNA

18:36 - December 22, 2008
Habari ID: 1721717
Shirika la Habari za Quran la Kimataifa IQNA limezindua rasmi huduma za habari kwa lugha ya Kiswahili. Shirika hilo lenye makao yake mjini Tehran Iran, limezindua ukurasa wake wa intaneti kwa lugha ya Kiswahili katika sherehe iliyohudhuriwa na maafisa waandamizi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha al Mustafa na wawakilishi wa Jihadi ya Vyuo Vikuu.
Akizungumza katika sherehe hizo, Rahim Khaki Mkurugenzi wa Shirika la Harakati za Quran la Wanachuo wa Iran amesema shirika la IQNA sasa linasambaza habari za Qur'ani kwa lugha ya Kiswahili. Amesema: Kwa mujibu wa mapatano kati ya Shirika la Harakati za Quran la Wanachuo wa Iran na Chuo Kikuu cha al Mustafa, shirika la habari la IQNA litakuwa linaanzisha huduma za lugha mbili mpya kila mwaka.
Akizungumza katika halfa hiyo, Kansela wa Chuo Kikuu cha al Mustafa Hujjatul Islamu A'rafi ameeleza matumaini yake kuwa mapatano kati ya taasisi hizo mbili yataimarisha uhusiano katika nyanja za utamaduni, elimu na utafiti. Huduma ya habari za Qur'ani kwa lugha ya Kiswahili ni ya 18 kuzinduliwa katika Shirika la Habari za Quran la Kimataifa IQNA. Huduma hiyo ya IQNA inatazamiwa kuwanufaisha wazungumzaji zaidi ya milioni 100 wa lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki na ya Kati na kwingineko duniani.
Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa IQNA ndilo la kwanza na pekee la aina yake ambalo linashughulikia kwa njia maalumu habari za Quran katika ulimwengu wa Kiislamu. Shirika la IQNA lilianzishwa tarehe 15 mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka 1424 Hijria sawa na 11 Novemba 2003 Miladia. 336656
captcha