Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa ya Amsterdam Uholanzi, Geert Wilders, mtayarishaji wa filamu ya Fitna inayokivunjia heshima kitabu kitukufu cha Qur'ani ambaye pia ni mwakilishi katika bunge la nchi hiyo atafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu.
Hukumu ya mahakama hiyo imesema: Geert Wilders ana hatia ya kuuvunjia heshima Uislamu na Waislamu kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kuwashabihisha Waislamu na manazi na kuchochea hisia za chuki.
Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Amsterdam amesisitiza kuwa, jamii ya kidemokrasia inapaswa kujiepusha na matamshi ya kejeli na uchochezi dhidi ya watu wengine.
Geert Wilders ndiye mtengenezaji wa filamu ya Fitna ambayo inaifananisha Qur'ani na kitabu cha "Mapambano Yangu" kilichoandikwa na dikteita wa zamani wa Ujurumani Hitler na kudai kuwa kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu ndio chanzo cha machafuko na utumiaji mabavu katika dini ya Kiislamu.
Awali juhudi za Waislamu za kumfikisha mahakamani Wilders ziligonga ukuta. 352284