IQNA

Kuchangia viungo vya mwili kwa mtazamo wa Qur'ani na hadithi

19:26 - February 22, 2009
Habari ID: 1747071
Suala la kuzawadia wagonjwa viungo vya mwili halijaashiriwa kwa njia ya wazi Katika Qur'ani Tukufu na hadithi za Watu wa Nyumba ya Mtume au Ahlul Bayt (as) .
Lakini kutokana na kuwa fiqhi ya Kiislamu ni pana na inaenda na wakati haijaliacha suala hili bila jawabu. Hii ni kwa sababu vyanzo vya fiqhi na istinbati yake au kutoa hukumu za kisheria kwa kutegemea vyanzo vya Kiislamu haviishii tu katika Qur'ani na hadithi, bali pia vinajumuisha akili kama kigezo kinachotumiwa na wanazuoni wa fiqhi.
Katika Qurian Tukufu na hadithi zilizopokelewa kutoka kwa Ahlul Bayt (as) hakupatikani aya au hadithi zinazoashiria suala hili moja kwa moja, kwani vyanzo hivyo viwili vimetoa muongozo wa kiujumla wa sheria kuu, wakati suala la kuzawadia mgonjwa viungo ni kati ya masuala yaliyojitokeza katika zama hizi za kisasa. Kwa sababu hiyo, suala hilo halikuzungumziwa kwa uwazi katika hadithi.
Katika Uislamu, kulinda maisha ya mwanadamu hasa Muislamu ni jambo linalopewa umuhimu mkubwa. Kwa hivyo baadhi ya wanazuoni wa fiqhi wanasema kuwa, iwapo kulinda maisha ya Muislamu kutategemea kupewa kiungo cha Muislamu aliyekufa, basi kukata kiunga hicho na kumpa anayehitajia ni jambo linalokubalika. Vivyo hivyo, suala hilo linajuzu iwapo kuhifadhi afya ya kiungo cha mwili wa Muislamu kutategemea kukatwa kiungo cha maiti, na maiti huyo akawa ameidhinisha suala hilo alipokuwa hai.*1
Qur'ani Tukufu inaashiria umuhimu wa kulindwa na kuheshimiwa maisha ya mwanadamu ambapo Mwenyezi Mungu baada ya kuashiria kuwa kumuua mwanadamu mmoja bila ya kuwa amefanya mauaji au ufisadi katika ardhi ni sawa na kuua wanadamu wote, anasema katika Qur'ani Tukufu kwamba: “Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote”. ( Al Maida 32)
Kwa hivyo kuchangia au hata kuuza vioungo vya mwili wa mwanadamu asiyekuwa hai na hata katika baadhi ya wakati viungo vya mwili wa mwanadamu aliye hai, ni katika vielelezo vya aya hiyo.
*1 Risala ya Taudhihul Masail ya Ayatullah Hussein Nuri Hamedani Uk. 610
366571
captcha