Hamid Ridha Mir Sanei, mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha al-Mustafa nchini Afghanistan amesema kuwa jumuiya hiyo imeweka wanafunzi wa Qur'ani wapatao 10,000 nchini Afghanistan chini ya ratiba zake za masomo.
Amesema, mwaka huu Qur'ani na vitabu vya mafunzo ya Qur'ani vimesambazwa na kutawanywa katika zaidi ya vituo 200 vya Qur'ani, maktaba na misikiti nchini humo.
Mir Sanei amesema mwaka huu chuo hicho kimetoa mafundisho kwa walimu wa Qur'ani wa daraja la kwanza wapatao 550 kutoka miji ya Mazar Sharif, Bamiyan na Kabul nchini Afghanistan.
Amesema, mbali na mafundisho ya Qur'ani, washiriki wa duru hii ya mafundisho pia walifundishwa masuala mbalimbali yanayohusiana na sheria na maarifa ya Kiislamu. Huku akiashiria kwamba mafundisho hayo ya Qur'ani ni ya kudumu nchini Afghanistan, amesisitiza kwamba nchi hiyo ina wasomaji wazuri sana wa Qur'ani na kwamba kuna mipango ya kuwaalika nchini Iran ili washiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa ya usomaji na kuhifadhi Qur'ani Tukufu. 370673