IQNA

Ulimwengu wa Kiislamu unapasa kupanua zaidi utafiti wa masuala ya Qur’ani

17:11 - April 08, 2009
Habari ID: 1762206
Kiwango cha utafiti wa masuala ya Qur’ani ni cha chini sana ikilinganishwa na utafiti uliofanywa hadi sasa kuhusiana na vitabu vingine vya mbinguni hususan Taurati na Injili, na kwa msingi huo ulimwengu wa Kiislamu unapasa kufanya jitihada kubwa zaidi za kustawisha na kupanua utafiti wa Qur’ani.
Hayo yamesemwa na Pr. Muhammad Adulhalim ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha London na msimamizi wa kongamano la Utafiti wa Masuala ya Qur’ani la chuo hicho.
Pr. Abdulhalim amesema kuwa kila mwaka wasomi na watafiti katika nchi mbalimbali za dunia hufanya utafiti kuhusu kitabu cha Injili na Taurati kwa lugha muhimu duniani, ilhali utafiti kama huo kuhusu Qur’ani hufanyika kwa lugha za Kiarabu, Kifarsi na lugha nyingine kadhaa tu. Amesema kuwa makala na vitabu vinavyoandika na wasomi wa Kiislamu kuhusu Qur’ani huzingatia zaidi mawaidha na ulinganiaji wa dini ya Kiislamu na kwa sababu hiyo havipewi umuhimu wa kutosha katika duru za kielimu za Magharibi.
Pr. Abdulhalim amevihimiza vyuo vikuu na vituo vya utafiti katika nchi za Kiislamu kutoa kipaumbele kwa suala la kuchapisha utafiti wao kwa lugha za Ulaya. Amesema, wasomi wa Kiislamu wanapasa kuwa na uoni mpana zaidi katika utafiti wa masuala ya Qur’ani na kufanya jitihada za kutambua maoni ya wasomi wasiokuwa wa Kiislamu katika uwanja huo. 384193
captcha