IQNA

Maulamaa wa Kiislamu watakiwa kujiepusha na maneno ya fitina

11:06 - June 23, 2013
Habari ID: 2550985
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amewataka maulama katika ulimwengu wa Kiislamu kujiepusha na matamshi yoyote ambayo yatapelekea kutokea fitina na mifarakano.
Ayatullah Muhsin Araki amesema hayo mjini Tunis siku Jumamosi katika kongamano la "Umoja wa Umma wa Kiislamu" linalofanyika kwa ushirikiano na ubalozi wa Iran nchini Tunisia. Amesisitiza kwamba, maadui wa Uislamu wanafanya njama za kusambaratisha umoja wa Umma wa Kiislamu na wamekuwa wakitumia njia ya kuzusha fitina na mifarakano kwa ajili ya kufikia malengo yao hayo.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amekosoa vikali misimamo ya uzushaji fitina na fatuwa za baadhi ya shakhsia ambao kidhahiri wanaonekana kuwa ni wa kidini katika ulimwengu wa Kiislamu. Amesisitiza kwamba, ni bora kwa Yusuf Qardhawi, Mkuu wa Muungano wa Maulama wa Kiislamu na wengine mfano wake badala ya kuchochea moto wa vita na umwagaji damu nchini Syria wawafanye watu wamzingatie adui wa kweli yaani utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wakati huo huo Rais wa Tunisia Moncef Marzouki siku ya Ijumaa alikutana na Ayatullah Araki mjini Tunis na kusema nchi yake inaunga mkono juhudi zote za kuwaleta pamoja na kuwakurubisha Waislamu duniani.
Rais Marzouki amepongeza Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu, yenye makao yake Tehran, kwa juhudi zake za kuleta umoja wa Kiislamu duniani.
Aidha ametaka uhusiano wa Tehran na Tunis uimarishwe pande zote na vile vile amepongeza uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni.
Siku ya Jumatano wiki iliyopita Rais Marzouki alisema rais mteule wa Iran Sheikh Hassan Rohani ana uwezo wa kutatua matatizo makubwa ya eneo na ulimwengu wa Kiislamu.

Katika mazungumzo ya simu na Rohani , Rais wa Tunisia alisema nchi yake ina matumaini makubwa kuwa rais mteule wa Iran atasaidia katika utatuzi wa matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu hasa kadhia ya Syria. Rais wa Tunisia alimpongeza Sheikh Rohani kwa ushindi wake katika uchaguzi na kumtakia mafanikio katika kazi zake.
Kwa upande wake, rais-mteule wa Iran alitoa wito wa kuimarishwa uhusiano baina ya nchi zote rafiki duniani ukiwemo uhusiano wa Iran na Tunisia.

1246208
captcha