IQNA

Mauaji ya Waislamu wa Kishia Misri na hasira za walimwengu dhidi ya jinai hiyo

12:29 - June 25, 2013
Habari ID: 2551849
Mauaji ya kutisha yaliyofanywa dhidi ya Waislamu wa Kishia katika kijiji cha Zawiyat Abu Muslim mkoani Giza nchini Misri yanaendelea kulaaniwa ndani na nje ya nchi hiyo.
Makundi mengi ya Misri pamoja na Chuo Kikuu cha al Azhar na viongozi rasmi wa nchi hiyo wameendelea kulaani mauaji ya Waislamu wanne wa Kishia katika kijiji hicho ambao baadaye vilivunjiwa heshima viwiliwili vyao na watu wenye misimamo mikali ya Kisalafi. Watu hao waliwashambulia kwa mawe na magongo Waislamu hao na kuwaua kikatili kabisa wakati Waislamu hao wa Kishia walipokuwa wanaadhimisha mkesha wa nusu ya Shaabani. Miongoni mwa Waislamu hao wanne waliouliwa kinyama na baadaye kuchomwa moto ni Sheikh Hassan Shehata. Kundi la Ikhwanul Muslimin limelaani jinai hiyo na kusema ni kitendo cha watu wenye fikra duni. Limesema, kundi hilo haliweza kunyamazia mauaji ya Mmisri yeyote yule na kama jeshi la polisi limeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda raia, basi liwape watu wengine kazi hiyo. Chuo Kikuu cha al Azhar nacho kimeitaja jinai hiyo kuwa ni katika "kabair" yaani madhambi makubwa sana na Shaikhul Azhar amelaani vikali jinai hiyo. Jinai hiyo imelaaniwa vikali pia nje ya Misri. Sheikh Muqtadas Sadr wa nchini Iraq amewataka Waislamu duniani kutangaza siku tatu za maombolezo kufuatia jinai hiyo ya kuuliwa Waislamu wanne wa Kishia akiwemo Sheikh Hassan Shehata huko nchini Misri. Chama cha Hizbullah cha Lebanon nacho kimelaani jinai hiyo. Nayo Jumuiya ya Kimataifa ya Kuyakurubisha pamoja Madhehebu ya Kiislamu imetoa tamko la kulaani mauaji hayo na kufichua kuwa, viongozi wa makundi yanayokufurisha Waislamu wengine wana orodha ya viongozi wa Kishia nchini Misri na wamekusudia kuwaua wote kikatili kama walivyofanya kwa Sheikh Hassan Shehata. Wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa wanaihesabu jinai ya kutisha iliyofanyika katika kijiji cha Zawiyat Abu Muslim mkoani Gizah nchini Misri kuwa ni jinai kubwa, bali ni fitna mbaya ambayo haijawahi kushuhudiwa mfano wake nchini Misri. Katika miezi ya hivi karibuni, makundi yenye misimamo mikali ya Kisalafi ambayo yanapata uungaji mkono kutoka kwa nchi kama Saudia na Qatar yamekuwa yakitekeleza hatua kwa hatua matakwa ya kibeberu ya Marekani. Vitendo vya makundi hayo vinalenga moja kwa moja kueneza fitna za kikabila na kidini katika nchi kama Syria, Iraq, Lebanon na sasa nchini Misri. Inaonekana wazi kuwa lengo la jinai hizo ni kutaka kuwatia vitani Waislamu wenyewe kwa wenyewe na hivyo kutoa nafasi kwa madola ya kibeberu kama Marekani kuwadhibiti zaidi Waislamu. Jambo la kujiuliza ni kuwa, wakati Muislamu anapoadhimisha matukufu ya Kiislamu kama kukesha kwa ibada katika usiku wa nusu ya Shaabani ni kosa? Na je, hukumu yake ni kuuawa? Na je, hukumu yake ni kufanyiwa ukatili na unyama kama waliofanyiwa Waislamu hao wanne wa Kishia na makundi yenye misimamo mikali ya Kisalafu huko nchini Misri? Ni jambo lililo wazi kabisa kuwa, dini tukufu ya Kiislamu haikubaliani hata kidogo na jinai kama hizo na kwamba sifa kubwa ya Uislamu ni kuvumiliana na kuishi salama na watu wote sambamba na kuilinda vilivyo dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo pia ndio maana weledi wa mambo wakaamini kuwa, jinai zinazofanywa na makundi hayo hayana uhusiano kabisa na Uislamu bali lengo lake pekee ni kutumikia malengo ya kibeberu ya madola kama Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Kuendelea kulaaniwa jinai zilizofanywa dhidi ya Waislamu wa Kishia katika kijiji cha Zawiyat Abu Muslim mkoani Gizah nchini Misri ni ushahidi wa wazi wa uovu mkubwa wa watenda jinai hao na kwamba mtu yeyote mwenye hisia za utu hawezi kamwe kukubaliana na jinai za watu hao.
1247605
captcha