Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Jumatano wakati alipokutana na mkuu na maafisa wa ngazi za juu wa Vyombo vya Mahakama. Mkutano huo umefanyika kwa mnasaba wa kuwadia kumbukumbu ya kuuawa shahidi Ayatullah Muhammad Beheshti na makada 72 wa Mapinduzi ya Kiislamu Juni 28 mwaka 1981 ambayo huadhimishwa kama Siku ya Vyombo vya Mahakama nchini Iran.
Katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu ameashiria hati iliyotiwa saini na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA ambapo wakala huo unakiri kuwa hakuna tatizo katika shughuli za kuzalisha nishati ya nyuklia za Iran na kwamba faili la nyuklia la Iran linapaswa kufungwa. Amesema punde baada ya kutiwa saini hati hiyo Marekani iliibua masuala mapya ili kutumia kadhia ya nyuklia kama njia ya kuitisha na kuishinikiza Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia uchochezi wa Wazayuni katika kadhia ya nyuklia ya Iran na kusema, 'katika kadhia ya nyuklia, Jamhuri ya Kiislamu inaendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria, kwa uwazi na kwa mtazamo wa dalili na ina mantiki yenye nguvu lakini malengo ya maadui ni kuendeleza mashinikizo, kulichosha taifa na kubadilisha mfumo wa utawala hapa nchini na kwa msingi huo hawataruhusu kadhia hii itatuliwe. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, kwa Wamagharibi shughuli za nyuklia, haki za binaadamu na demokrasia ni vitu visivyo na maana na kile wanachofuata ni kuzuia ustawi wa taifa na kueneza tena ubeberu wao nchini Iran lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uwezo, uhuru kamili, kutegema wananchi na kutawakali kwa Allah, imesimama kidete na italinda maslahi yake.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amepongeza hamasa adhimu na ya hakika ya taifa erevu na lenye uono wa mbali la Iran katika uchaguzi wa Juni 14. Ameongeza kuwa siri ya kushiriki kwa wingi taifa katika uchaguzi wa mwaka huu ni imani na mapenzi yao kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, imani kwa wasimamizi wa uchaguzi na matumaini ya taifa kuhusu ustawi wa Iran. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa kuna udharura wa kumsaidia rais-mteule na kuongeza kuwa, njama za maadui zimefeli katika pande zote. Aidha amesifu hatua ya wagombea wote kumpongeza rais-mteule na kusema jambo hilo linaashiria utiifu wao kwa sheria pamoja na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu. Kiongozi Muadhamu amesema pamoja na kuwa serikali inayoondoka ina udhaifu lakini pia ina nukta za nguvu na hivyo wagombea urais pamoja na kuashiria nukta za udhaifu wangepaswa pia kutaja mafanikio yaliyopatikana hasa katika ustawi wa miundo msingi.
1248534