Akizungumza katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mjini Tehran, Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran amesema uwepo wa utawala wa Kizayuni wa Israel unatokana na uongo mkubwa wa kihistoria na ushirikiano wa madola yenye kiburi kwa lengo la kuikoloni dunia.
Amesema utawala bandia wa Israel ni nukta ya pamoja na madola yote ya kibeberu ambayo yanataka kulinda maslahi yao haramu. Ameongeza kuwa mataifa huru duniani kamwe hayatafumbia jicho Palestina ambayo ni ardhi inayoshuhudia maangamizi ya umati na uporaji wa utajiri wake. Rais wa Iran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unahusika na jinai katika nchi zote za eneo na kuongeza kuwa eneo la Mashariki ya kati lina utajiri mkubwa wa nishati na ndio sababu madola ya kibeberu yanaunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel kwa lengo la kudhamini maslahi yao haramu. Ahmadinejad ametoa wito kwa Waislamu duniani wawe macho mbele ya njama za madola ya kibeberu na Wazayuni na kusema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuwaunga mkono Wapalestina. Mamillioni ya Wairani wamejitokeza kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Quds huku wakiwa na mabango na wakitoa nara dhidi za 'Mauti kwa Marekani' na 'Mauti kwa Israel' sambamba na kutangaza kufungamana kwao na taifa linalodhulumiwa la Palestina. Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds pia yamefanyika katika nchi nyingi duniani Ijumaa hii.
Kwingineko Rais-mteule wa Iran Dkt. Hassan Rohani ameashiria umuhimu wa maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kusema siku hii ni siku ya Waislamu kuonyesha umoja wao na mapambano yao dhidi ya dhulma. Akizungumza leo Ijumaa alipojiunga na Mamillioni ya Wairani katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mjini Tehran, Rohani amesema maandamano hayo ni uungaji mkono wa kisiasa na kimaanawi kwa watu wa Palestina ambao wanapambana kuikomboa Quds Tukufu. Dkt. Rohani amesema: "Katika eneo kuna kivuli cha ukaliwaji kwa mabavu ardhi ya Palestina na Quds Tukufu, ni kidonda kilicho katika mwili wa ulimwengu wa Kiislamu." Ameongeza kuwa siku ya Kimataifa ya Quds ni mirathi ya Imam Khomeini na kwamba ni 'kumbusho kuwa Waislamu kamwe hawatashau haki yao ya kihistoria ya kupinga dhulma na uvamizi.'
Kuhusu kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, Dkt. Rohani amesema: "Katika hali ambayo hivi sasa ulimwengu wa Kiislamu katika eneo umekumbwa na matatizo, Wazayuni wanafikiri ni fursa bora kuhadaa kuwa wanataka amani wakati uhalisi wa mambo ni kuwa wanaendeza hujuma zao dhidi ya Wapalestina."
Mapema baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vimepotosha matamshi ya Dkt. Rohani na kudai kuwa amesema Israel inapaswa kuangamizwa.
1266945