IQNA

Mapinduzi ya Kijeshi Sudan na mustakabali wa nchi hiyo

13:53 - October 26, 2021
Habari ID: 3474475
TEHRAN (IQNA)- Baada ya kupita siku 33 tangu kutokea jarIbio la mapinduzi lililofeli nchini Sudan, mapinduzi mapya ya kijeshi yametokea katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Usiku wa kuamkia jana Jumatatu, vikosi vya jeshi vilimtia mbaroni Waziri Mkuu Abdalla Hamdok na wawakilishi wa kiraia wa baraza la uongozi wa mpito la Sudan na mawaziri kadhaa wa serikali ya mpito ya nchi hiyo. Masaa machache baada ya habari ya kutokea mapinduzi hayo, Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan, aliyekuwa kiongozi wa baraza la pamoja na viongozi wa kiraia, alijitokeza na kutangaza kuwa, jeshi la Sudan limevunja serikali ya mpito iliyokuwa inajumuisha raia na wanajeshi, na wakati huo huo kuwakamata viongozi wa kisiasa akiwemo Waziri Mkuu Abdalla Hamdok na kutangaza hali ya hatari nchi nzima. Mkabala na tangazo hilo, Abdalla Hamdok ametoa ujumbe akiwa katika sehemu anayoshikiliwa ambapo amewataka wananchi wa Sudan waheshimu amani na wajitokeze katika mitaa na barabara za nchi hiyo kwa ajili ya kutetea mapinduzi yao.

Njama ya kurejesha utawala wa kidikteta

Wapinzani wa jeshi wanawatuhumu viongozi wa kijeshi kwamba, wanafanya njama za kurejesha utawala wa kidikteta nchini Sudan. Viongozi wa jeshi na raia wamekuwa wakizozana tangu kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir kupinduliwa miaka miwili iliyopita na serikali ya mpito kuanzishwa. Muhammad al-Taayushi, mjumbe wa Baraza la Utawala nchini Sudan amesema, kile kilichotrokea nchini humo ni usaliti na ametoa mwito kwa wananchi wa Sudan kuendesha muqawama na mapambano ya amani.

Mmoja wa makamanda wa kijeshi nchini Sudan alitangaza adhuhuri ya jana kwamba, serikali imevunjwa na kwamba, muda si mrefu kutaundwa Baraza la Mawaziri kutoka miongoni mwa shakhsia wastahiki. Mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan yametokea siku mbili tu baada ya Jeffrey Feltman, mjumbe maalumu wa Marekani katika eneo la Pembe ya Afrika kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kijeshi na kiraia wa Sudan.

Maandamano ya wananchi

Katika majuma ya hivi karibuni, Sudan imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa yanayolalamikia hali mbaya ya kiuchumi na kijamii ya nchi hiyo. Maelfu ya wakazi wa mji mku Khartoum hivi majuzi walifanya maandamano makubwa mjini humo ambapo sambamba na kuinyooshea kidole cha lawama serikali ya mpito kwamba, ndio chanzo cha kusambaratika uchumi na mwenendo wa kisiasa  nchini humo, walitoa wito wa kuvunjwa serikali hiyo. Kimsingi ni kuwa, mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan yametokea baada ya wiki kadhaa mivutano baina ya serikali ya mpito na jeshi.

Uhusiano na Israel wapingwa

Mbali na kulalamikia utendaji mbovu wa serikali ya mpito, jambo jengine lililokuwa likilalamikiwa na wapinzani ni hatua ya serikali ya Khartoum ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, hatimaye Sudan ilisalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani na kukubali kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Sudan ilikuwa na matumaini ya kupata misaada ya kiuchumi kutoka kwa Marekani baada ya kufuata mkumbo wa kuanzisha uhusiano na kawaida na Tel Aviv. Hata hivyo inaonekana matumaini yake yameota mbawa; kwani kinyume na ahadi zake Washington haijaipatia Sudan misaada hiyo.

Matatizo ya kiuchumi

Ukweli wa mambo ni kuwa, mgogoro wa Sudan ulishtadi zaidi baada ya kuongezeka matatizo ya kiuchumi na mizozo y kisiasa. Ilikuwa ikitabiriwa tangu awali kwamba, kkutokana na historia ya nchi hiyo ya kutokea mapinduzi, mara hii pia kungetokea mapinduzi mengine, utabiri ambao sasa umetimia.

Sudan ilitumbuukia katika vita vya kuwania madaraka baina ya wanajeshi na wanasiasa na wawakilishi wa asasi za kiraia, Apiri 2019 baada ya kuondolewa madarakani Omar Hassan al-Bashir. Kimsingi ni kuwa, Sudan ilishuhudia kushadidi mpasuko baina ya mirengo shindani ambayo ilichukua hatamu za uongozi baada ya kuondolewa madarakani Omar al-Bashir. Sudan ambayo ni ya tatu kwa ukubwa wa kimasafa barani Afrika, iliingia katika kipindi cha utawala wa mpito kuanzia Agosti 21 mwaka 2019 ambapo kilitarajiwa kuendelea kwa miezi 53 na kisha kuitishwa uchaguzi mwaka 2024. Kabla ya mapinduuzi ya jana Jumatatu, madaraka ya nchi yalikuwa yamegawanywa baina ya jeshi na Muuungano unaojulikana kama al-Hurriyah Wat-Taghir (Uhuru na Mageuzi).

Giza totoro

Filihali baada ya mapinduzi haya mapya, mustakabali wa Sudan unakabiliwa na giza totoro. Kwa kuzingatia kwamba, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Marekani zimepinga mapinduzi hayo na kutoa wito wa kuachiliwa huru Wazri Mkuu Abdalla Hamdok na viongozi wengine wanaoshikiliwa kizuizini, wafanyamapinduzi ambao kidhahiri wanaungwa mkono na Abdul-Fatah al-Burhan, aliyekuwa Kiongozi wa Baraza la Utawala la Sudan bila shaka watakuwa na kibarua kigumu hasa kwa kuzingatia ghasia na machafuko ambayo tayari yameibuka na kupelekea kuuawa watu kadhaa.

Hivi sasa macho na masikio ya walimwengu yameelekea Sudan yakisubiri kuona au kusikia kama je, wafanyamapinduzi watalegeza msimamo kutokana na mashinikizo na upinzani wa kimataifa au wataendelea kung'ang'ania msimamo wao wa kutaka kuunda serikali mpya?

84517011

Kishikizo: sudan burhan hamdok
captcha