IQNA

Maafisa wa kijasusi wa Israel wakutana na waliopindua serikali Sudan

18:57 - November 03, 2021
Habari ID: 3474510
TEHRAN (IQNA)- Ujumbe wa utawala wa Kizayuni wa Israel unaripotiwa kuitembelea Sudan kwa siri na kificho, muda mfupi baada ya kujiri mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Oktoba 25 mwaka huu katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Duru za habari zinaarifu kuwa, ujumbe wa Wazayuni ulioenda Sudan baada ya kujiri mapinduzi hayo ulijumuisha maafisa wa Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel (Mossad).

Ujumbe huo ulikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kijeshi wa Sudan akiwemo Jenerali Abdel Rahim Hamdan Dagalo, kamanda wa ngazi ya juu wa Kikosi cha Usaidizi wa Dharura kilichoongoza mapinduzi hayo.

Gazeti la Kizayuni la Times of Israel limedai kuwa, ujumbe huo uliitembelea Sudan eti kwa ajili ya kutathmini kwa karibu matukio yaliyojiri na namna yangeweza kuathiri jitihada za kusainiwa makubaliano ya mwisho ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya Tel Aviv na Khartoum.

Hata hivyo wadadisi wa mambo wanaamini kuwa, safari hiyo ya ujumbe wa Israel mjini Khartoum inaashiria kuwa huenda Tel Aviv ilihusika na mapinduzi hayo, kwa lengo la kutaka kuweko mtawala rafiki kwa Wazayuni Sudan. 

Baada ya kujiri mapinduzi ya kijeshi huko Sudan, Waziri Mkuu, Abdallah Hamdok na mawaziri wengine kadhaa wa serikali ya mpito ya nchi hiyo waliwekwa kizuizini.

Aidha Jenerali Abulfattah Al Burhan alitangaza hali ya hatari huko Sudan na kuvunja Baraza la Uongozi la nchi hiyo ambalo analiongoza yeye.  

Hayo yanajiri wakati ambao wananchi wa Sudan wamefanya maandamano mara kadhaa kupinga vikali uhusiano wa nchi yao na utawala wa Israel. Katika maandamano hayo wananchi wenye hasira wamekuwa wakiteketeza bendera za utawala huo wa Israel ambao unazikoloni na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina ukiwemo mji wa Quds (Jerusalem) uliko Msikiti Mtakatifu wa Al Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na eneo la tatu takatifu zaidi katika Uislamu.

4009901/

captcha