IQNA

Ndege kutoka Saudia kutua Israel kwa mara ya kwanza

18:31 - October 25, 2021
Habari ID: 3474469
TEHRAN (IQNA)- Kwa mara ya kwanza, ndege ya moja kwa moja kutoka Ufalme wa Saudi Arabia inatazamiwa kutua leo Jumatatu usiku katika katika utawala bandia wa Israel.

Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa, ndege hiyo ya shirika la Emirati la Royal Jet itatua usiku huu katika Uwanja wa Ndege wa Ben-Gurion ikitokea Riyadh, katika hatua ambayo kwa mara nyingine tena inadhihirisha jitihada za utawala wa kifalme wa Saudia na utawala wa Kizayuni wa Israel za kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Haya yanajiri baada ya Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Ikulu ya White House ya Marekani kumshinikiza Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 2018, Saudi Arabia ilifungua anga yake kwa mara ya kwanza na kuziruhusu ndege za shirika la Air India kutumia anga hiyo katika safari zake za kwenda na kutoka Israel.

Kabla ya hapo, Muhammad bin Salman alifanya safari za siri huko Israel ambapo alikutana na viongozi wa ngazi za juu wa utawala huo haramu unaozikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Wadadisi wa mambo wanasema hatua hizi za Riyadh zinalenga kuandaa mazingira ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, ikifuata mkumbo wa Imarati, Bahrain, Morocco na Sudan.

Miongoni mwa njama hizo za Saudia ni mpango wake wa kuitambua rasmi Israel uliopendekezwa na Riyadh mwaka 2002. Mpango huo wa Saudia ulipuuza haki nyingi na za kimsingi za Wapalestina ndio maana umeshindwa. Vile vile njama za Saudi Arabia na Israel za kujaribu kuivunja nguvu kambi ya muqawama na pia kuunga mkono kwao magenge ya kigaidi katika eneo hili, zimezidi kufichua muundo wao halisi  wa kwamba madola hayo mawili ndiyo tishio la kweli la amani, usalama na utulivu wa kimataifa.

4007864

Kishikizo: saudia israel
captcha