IQNA

Sudan yasema haiafiki Israel kuwa mwangalizi katika Umoja wa Afrika

17:38 - October 15, 2021
Habari ID: 3474424
TEHRAN (IQNA)- Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imetangaza kuwa nchi hiyo inapinga utawala wa Kizayuni wa Israel kupewa hadhi ya mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika.

Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesema: "Sisi tunapinga uamuzi wa Tume ya Umoja wa Afrika kuipa Israel hadhi ya mwanachama mwangalizi bila mashauriano na nchi wanachama kwani hatua hii itapelekea kuwepo hitilafu baina ya mwenyekiti wa tume na nchi wanachama."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa muelekeo kama huo unapingwa na ni kinyume cha misingi ya Umoja wa Afrika inayosisitiza kuhusu ushirikiano na kuheshimiana.

Mwezi Julai mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alitangaza kuwa tume hiyo imeafikia utawala wa Kizayuni wa Israel uwe mwanachama mwangalizi wa umoja huo. Uamuzi huo umepingwa vikali na nchi nyingi wanachama wa umoja huo. Aghalabu ya nchi zinazopinga zinasema  Israel kuwa mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika ni kinyume cha maazimio ya umoja  huo kuhusu kuunga mkono harakati za ukombozi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Algeria inaongoza kundi la nchi zaidi ya 15 ambazo zinapinga Israel kuwa mwanachama mwangalizi wa Umoja wa  Afrika na imeonya kuwa yamkini umoja huo ukasambaratika iwapo uamuzi huo hautabatilishwa.

4005093/

captcha