IQNA

Waziri Mkuu wa Pakistan

Umoja wa Mataifa uunde muungano wa kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu

20:59 - September 26, 2020
Habari ID: 3473203
TEHRAN (IQNA)- Waziri Mkuu wa Pakistan ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuunda muungano wa kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu au Islamophobia.

Imran Khan alisema hayo jana Ijumaa katika hotuba aliyoitoa katika mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea kufanyika kwa njia ya intaneti kupitia mawasiliano ya video, ambapo amelaani vikali kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW huku akitoa wito wa kuwepo jitihada za kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu duniani.

Aidha Waziri Mkuu wa Pakistan amesema serikali ya Kihindu ya India inaunga mkono na kuchochea chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo.

Imran Khan ameikosoa serikali ya New Delhi kwa kuchukua hatua za kuimarisha udhibiti wake katika eneo lenye Waislamu wengi la Kashmir.

Amesema harakati za chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) zimekita mizizi nchini India na kuhatarisha maisha ya Waislamu zaidi ya milioni 200 wa nchi hiyo ya Asia.

Khan amesema: "Nasikitika kusema kuwa, hii leo nchi moja duniani ambayo dola linafadhili chuki dhidi ya Uislamu ni India. Haya yote yametokana na idiolojia (potofu) ya RSS inayotawala (India). Wanaitakidi kuwa India ni mahususi kwa Wahindu pekee, na raia wengine hawana haki."

Waziri Mkuu wa Pakistan amesema amani ya kudumu na uthabiti havitashudiwa Kusini mwa Asia hadi pale mgogoro kuhusu maeneo ya Kashmir na Jammu utakapopatiwa ufumbuzi kwa kutegemea misingi ya sheria za kimataifa. Mwezi Agosti mwaka jana, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi alibatilisha mamlaka ya kujitawala eneo la Kashmir hatua ambayo Pakistan iliitaja kuwa kinyume cha sheria.

Imran Khan ameitaka jamii ya kimataifa ichunguze ugaidi wa kiserikali na jinai za kutisha na zinazokanyaga haki za binadamu zilizofanywa na raia na maafisa usalama wa India dhidi ya Waislamu wa maeneo ya Jammu na Kashmir katika maandamano ya kulaani sheria hiyo tata.

3925399

captcha