IQNA

Ayatullah Nouri Hamedani

Qur’ani Tukufu inavunjiwa heshima kwa himaya ya Marekani na Israel

11:21 - September 06, 2020
Habari ID: 3473142
TEHRAN (IQNA)- Mwanazuoni wa ngazi za juu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu ni njama za vituo vya kifikra vya Utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani katika fremu ya kueneza chuki na hofu dhidi ya Uislamu.

Ayatullah Hossein Nouri-Hamedani, amesisitiza kuwa, kuna haja ya Waislamu kuungana na kuwa na mshikamano baina yao kwa ajili ya kusimama kidete mbele ya mipango michafu kama hii.

Marjaa huyo wa kidini sambamba na kulaani hatua ya kuivunjia heshima Qur'ani Tuukufu ameeleza kuwa, hatua hiyo ya aibu na fedheha imezijeruhi nyoyo za watu wote huru duniani.

Ayatullah Nouri Hamedani amewataka viongozi wa mataifa ya Kiislamu pamoja na asasi za kimataifa kutoa majibu yao makali dhidi ya hatua hii na kuzuia kukaririwa vitendo kama hivi ambavyo vinajeruhi na kuumiza hisia za Waislamu.

Hivi karibuni, watu wenye chuki dhidi ya Uislamu walichoma moto na kuteketeza nakala ya Qur'ani katika mji wa Malmo nchini Sweden. Walioivunjia heshima Qurani Tukufu nchini Sweden ni wafuasi wa mwanasiasa mwenye misimamo mikali ya kibaguzi wa Denmark, Rasmus Paludan.

Hivi karibuni, watu wenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu walifanya maandamano katika mji mkuu wa Norway, Oslo huku mmoja wao akionekana akichana kurasa za Qurani Tukufu na kuzitemea mate.

Aidha, wafuasi wa mwanasiasa Rasmus Paludan, ambaye anaongoza chama cha chenye misimamo mikali cha mrengo wa kulia ambacho kinapinga Waislamu huko nchini Sweden, walijumuika kinyume cha sheria mjini Malmo na kukivunjia heshima Kitabu Kitukufu cha Waislamu.

Si hayo tu, lakini pia gazeti la maadui wa Uislamu la Charlie Hebdo la nchini Ufaransa, siku ya Jumanne iliyopita lilifanya utovu wa adabu mpya wa kuchora vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW. Vitendo hivyo ambavyo vimefanyika katika fremu ya chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) vinaendelea kulaaniwa kote duniani.

3921050

captcha