IQNA

Rais Rouhani

Marekani haina budi ila kusalimu amri mbele ya Iran

16:45 - February 18, 2021
Habari ID: 3473662
TEHRAN (IQNA) -Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, leo hii Marekani na serikali mpya ya nchi hiyo zimetambua kuwa zilifanya makosa kuhusu Iran na kueleza kuwa: Kusalimu amri mbele ya sheria si aibu na kwamba serikali ya Marekani haina budi ila kusalimu amri mbele ya sheria.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye alikwua akizungumza katika uzinduzi wa miradi ya kitaifa ya sekta za viwanda na madini katika mikoa mitatu ya Hormozgan, Kerman na Mazandaran amesema siku hizi kunaenezwa propaganda kwamba, Iran imechukua hatua kwa lengo la kuishinikiza Marekani; maneno haya si sahihi. Kile tunachokitaka sisi ni kutekeleza sheria na majukumu. 

Rais Rouhani ameeleza kuwa, kuheshimu sheria na majukumu ya kimataifa na kuyatekeleza ni miongoni mwa nyadhifa za kibinadamu na kisiasa wa serikali zote. Amesema: Tunataraji viongozi wa Marekani watarejea katika sheria na kuheshimu ahadi na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati huo huo ameashiria uwekezaji wa zaidi ya tumani bilioni elfu nane na mia tano katika miradi na shughuli ambazo zimezinduliwa hii leo na kubainisha kuwa: Kuzinduliwa miradi hiyo ya kitaifa ni ishara ya kuongezeka uzalishaji.  

Mazungumzo na Kansela wa Ujerumani

Wakati huo huo, Rais Rouhani amesema ni jambo lisilowezekana kuarifisha na kujumuisha maudhui nyinginezo katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Katika mazungumzo yake ya simu na Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani jana Jumatano, Rais Rouhani alizikosoa nchi za Ulaya kwa kufeli kutekeleza majukumu yao ndani ya JCPOA baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo.

Ameeleza bayana kuwa, "JCPOA ina fremu maalumu isiyobadilishika, na iwapo Ulaya inataka kuyalinda mapatano hayo kikweli, lazima idhihirishe hilo kivitendo." Baadhi ya nchi za Ulaya zinataka kujumuishwa uwezo wa makombora wa Iran na ushawishi wa taifa hili katika eneo la Asia Magharibi kwenye mapatano hayo ya kimataifa, miito ambayo Tehran imeyapuuzilia mbali.

Rouhani amesisitiza kuwa, Marekani itakapoiondolea Iran vikwazo haramu na kurejea katika Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, basi Jamhuri ya Kiislamu itarejea mara moja katika utekelezaji wa wajibu wake katika mapatano hayo.

Amesisitiza kuwa, serikali ya Tehran ina jukumu la kupunguza uwajibikaji wake ndani ya mapatano hayo kwa mujibu wa sheria iliyopasishwa na Bunge la Iran na kwamba kwenda kinyume na hayo, ni kukanyaga sheria za nchi.

Kadhalika Rais Rouhani katika mazungumzo yake ya simu na Kansela wa Ujerumani ametoa mwito wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili wa Iran na Ujerumani katika nyuga mbalimbali hususan kuimarishwa ushirikiano wa makampuni na sekta binafsi za nchi mbili hizi.

Kwa upande wake, Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani amesisitizia udharura wa kuilinda JCPOA kama mapatano ya kimataifa, huku akitoa mwito wa kupatia ufumbuzi tofauti zilizopo kupitia njia za mazungumzo. Amesema kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa pande zote husika ni kwa maslahi ya usalama na uthabiti wa eneo zima.

3954818

Kishikizo: iran jcpoa rouhani
captcha