IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
18:53 - February 17, 2021
Habari ID: 3473659
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameashiria hotuba yake ya hivi karibuni kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baina ya Iran na nchi tano za kundi la 5+1 na kusema kuwa: Iwapo upande mwingine utatekeleza makubaliano hayo, Iran pia itatekeleza vipengee vyake, na mara hii Jamhuri ya Kiislamu haitatosheka kwa maneno na ahadi tupu.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo mapema leo katika hotuba yake kwa njia ya video akizungumza na wananchi wa Tabriz huko magharibi mwa Iran. Ameongeza kuwa: Kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kunasemwa maneno na kutolewa ahadi, lakini tumesikia maneno na ahadi nyingi zinazokiukwa; kwa msingi huo maneno na ahadi tupu hazina faida yoyote na mara hii vitendo ndivyo vitakavyopewa mazingatio."

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa hatupasi kusahau sababu kuu za uadui wa mabeberu dhidi ya Mapinduzi na Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Mabeberu wamekuwa wakitekeleza njama na uadui wao kwa kutumia visingizio vya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na suala la haki za binadamu, sheria za Kiislamu, kadhia ya nyuklia, makombora ya Iran na masuala mengineyo, lakini inatupasa kuelewa kuwa masuala haya yote ni visingizio tu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kuimarika nguvu za kijenzi na kiulinzi, na kubadilika kwa Iran na kuwa nguvu kubwa ya kikanda ni miongoni mwa matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Ameongeza kuwa, sababu kuu ya njama za aina mbalimbali za Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za Ulaya dhidi ya Iran ni harakati hii inayosonga mbele ya maendeleo, na kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, nguvu ya wananchi na viongozi itashinda na kuvunja njama hizo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria uchaguzi ujao wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema, uchaguzi ni fursa kubwa kwa taifa. Ameongeza kuwa: Hata hivyo wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu hawataki kuona utawala wa Kiislamu ukitumia fursa hiyo kwa ajili ya maendeleo ya nchi; lakini ushiriki mkubwa na wa kimapinduzi ya wananchi katika zoezi hilo utazidisha usalama wa taifa, kutoa pigo kwa maadui na kupunguza tamaa ya maadui.    

3954580

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: