IQNA

Ulazima wa kuandaliwa mazingira ya kubadilishana mawazo kati ya wataalamu wa Qur'ani katika mashindano ya Qur'ani ya wanachuo

12:26 - November 08, 2008
Habari ID: 1705684
Uwanja unaofaa wa kufanyika mazungumzo na kubadilishana mawazo kati ya wataalamu wa masuala ya Qur'ani unapaswa kuandaliwa katika awamu ya pili ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya wanachuo wa nchi za Kiislamu.
Hayo yamesemwa na Hujatul Islam wal Muslimeen Ali Ridha Araqi, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Mustafa alipokuwa akizungumza katika mahojiano na mwandishi wa Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa IQNA na kuongeza kuwa, kuna udharura wa kutekelezwa mipango mingine ya Kiislamu pambizoni mwa mashindano hayo. Amesema, kuandaliwa mazingira ya kufanyika mazungumzo na kubadilishana mawazo kati ya wageni na wataalamu wa Qur'ani katika vikao maalumu pambizoni mwa mashindano hayo ni jambo zuri linaloweza kunyanyua nafasi ya Qur'ani ulimwenguni. Amesema kufanyika maonyesho ya bidhaa zinazotengenezwa katika nchi za Kiislamu na vilevile kufanyika vikao vya washindani wa Qur'ani pembeni ya mashindano hayo ni mipango muhimu na ya kuvutia ambayo inaweza kutekelezwa katika mashindano hayo.
Hujjatul Islam Araqi ameendelea kusema kuwa, Qur'ani ni kamba inayouunganisha umma wa Kiislamu na utambulisho wa pamoja wa umma huo na kwamba kutokana na hilo, uenezwaji wa mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu na kila jambo linalohusiana nacho, ni thamani muhimu na ya kimsingi. Amesisitiza kwamba thamani hiyo ni nguzo muhimu inayoweza kuchukuliwa kuwa muhimili thabiti wa kuwaunganisha Waislamu na kuleta umoja miongoni mwao. Akiashiria umuhimu wa kufanyika mashindano ya Qur'ani ya wanachuo wa nchi za Kiislamu, Hujjatul Islam wal Muslimeen Araqi amesema ni wazi kuwa mashindano hayo yanaimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu na kuwashajiisha vijana wazingatie zaidi mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu. Araqi ameashiria kushiriki kwa wanachuo wa Kiislamu wanaotoka katika nchi zisizo za Kiislamu katika mashindano hayo na kusema kuwa jambo hilo linaweza kusaidia sana katika kueneza thamani za Kiislamu katika nchi hizo. 313959
captcha