Kwa mujibu wa tovuti ya almesryoon, al-Qadhi amesema kuwa sheria nambari 102 ya mwaka 1985 haina uwezo wa kuzuia uzembe katika uchapishaji na usambazaji wa Qur'ani Tukufu wala njama za baadhi ya watu wanaotaka kupotosha mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu. Kwa msingi huo amesema ameona kwamba kuna haja ya kuwasilisha sheria nyingine bungeni ambayo itazuia tatizo hilo.
Al Qadhi Amesema hatua yake hiyo imechochewa pia na hatua ya baadhi ya mashirika kuchapisha nakala za Qur'ani zilizo na makosa ya chapa. Ameongeza kuwa suala hilo linabainika wazi katika hatua ya Jumuiya ya Utafiti wa Kiislamu ya al-Azhar ya kukusanya karibu nakala 20,000 za Qur'ani zilizokuwa na makosa ya chapa kwenye aya, maneno na kurasa zake.
Bwana al-Qadhi amesema mashirika mengi ya uchapishaji Qur'ani nchini Misri hayana vibali vya kuchapisha kitabu hicho cha mbinguni na kwamba huwa hayajali, kuchunguza wala kudhibiti kwa makini nakala za Qur'ani zinazochapishwa kabla na baada ya uchapishaji wake. Amesema kwa kawaida nchini Misri mashirika mengi huzidisha shughuli zao za kuchapisha Qur'ani katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kwa mujibu wa mswada huo kifungo cha miaka 15 jela na faini kubwa ya pesa kimeainishiwa watu wanaopotosha kwa makusudi maandishi ya Qur'ani wakati wa uchapishaji. 998789