IQNA

Rais wa Ujerumani atembelea msikiti, atoa wito wa heshima baina ya dini

13:48 - December 03, 2019
Habari ID: 3472252
TEHRAN (IQNA)- Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani Jumatatu ametembelea msikiti katika mji wa Penzberg na kutoa wito wa kuwepo hali ya kuheshimiana baina ya wafuasi wa dini mbali mbali.

Steinmeier amesema kuheshimiana wafuasi wa  dini mbali mbali ni muhimu hasa katika kipindi hiki ‘wakati tunashuhudia ongezeko la mgawanyiko katika jamii yetu, ambapo pia kuna chuki kubwa.’

Akizungumza wakati alipomtembelea imamu wa msikiti wa eneo hilo, Sheikh Binyamin Idriz, amesema kile kinachojiri huko Penzberg na hasa katika msikiti huo ndicho kinachotakikana Ujerumani. Ametoa wito kwa watu wote Ujerumani kuheshimiana na kuongeza kuwa: “Kuhusiana na nukta hii, kile kinachojiri hapa ndicho tunachotaka; watu wa dini mbali mbali wanaishi pamoja na wanaheshimiana. Hivi ndivyo watu wa Penzberg wanavyoishi.”

Rais wa Ujerumani ameipongeza jamii wa Kiislamu huko Penzberg na pia wakazi wengine wa mji huo kwa kuikumbatia jamii ya Kiislamu.

Steinmeier amesema mji wa Penzberg unaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii nyingi, hasa katika miji mikubwa.

Wakati wa safari ya Steinmeier, watu kadhaa waliandamana wakitoa wito wa kuwepo hali ya kustahmiliana zaidi na maelewano baina ya watu wa dini na tamaduni mbali mbali. Aidha watu wanaounga mkono kijikundi cha mrengo wa kulia chenye misimamo mikali ya kibaguzi, PEGIDA, waliandamana siku hiyo lakini idadi yao ilikuwa ndogo sana.

Katika miaka ya hivi karibuni Ujerumani imeshuhudia ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu kutokana na propaganda za vyama vya mrengo wa kulia vyenye chuki kama vile PEGIDA.

3470021

 

captcha