IQNA

Waislamu katika mpaka wa Poland-Belarus wasaidia wakimbizi

19:39 - November 28, 2021
Habari ID: 3474611
TEHRAN (IQNA) – Waislamu katika kijiji cha Bohoniki nchini Poland sasa wanaongoza mkakati wa kuwasaidia wakimbizi katika eneo hilo linalopakana na Belerus.

Katika wiki za hivi karibuni kumekuwa na mgogoro mkubwa wa maelfu ya wakimbizi katika mpaka wa Poland na Belarus ambapo aghalabu ya wakimbizi waliofika hapo ni Waislamu wanaokimbia vita au migogoro katika nchi zao za Mashariki ya Kati hasa Iraq, Syria na pia Afghanistan.

Hivi sasa Waislamu wa Bohoniki wanawapatia misaada wakimbizi hao na hadi wameweza kuwazika waislamu wanne ambao wamefariki wakiwa wanajaribu kuvuka mpaka kutoka Belarus.

Rais Alexander Lukashenko wa Belarus amesema Marekani inatumia mgogoro wa wakimbizi kutaka kuibua makabiliano baina ya nchi mbili hizo. Rais Lukashenko amesema Washington imeazimia kuanzisha vita nchini Belarus kwa kuyatumia mataifa ya Poland, Ukraine na nchi za eneo la Baltic.

Huku madola makubwa yakiendelea kuzozoana kuhusu wakimbizi hao, Waislamu wa jamii ya Tatar mashariki mwa Poland wamewasaidia wakimbizi hao kupata nguo na chakula wakati huu wa msimu wa baridi kali.

Bango katika msikiti wa kijiji hicho lina maandishi yanayosema kuwa Waislamu wa Poland wanajiunga na jeshi la nchi hiyo katika kuwasaidia wakimbizi.

Kijiji cha Bohoniki kina moja ya jamii kongwe zaidi za Waislamu barani Ulaya. Kijiji hicho ambacho kiko kilomita 15 kutoka mkapa wa Belarus kilikabidhiwa Waislamu wa jamii ya Tatar na mfalme mwenye kushukuru wa Poland miaka 300 iliyopita baada ya wapiganaji wa Tatari kutoka Crimea kusaidia katika kulinda mipaka ya nchi hiyo.

Rais wa zamani wa Boland Bronislaw Komorowski amesema damu ya Waislamu hao wa jamii ya Tatar ilisaidia kuunda Jamhuri ya Poland.

Mufti wa Waislamu wa Poland, Tomasz Miśkiewicz amesema bila kujali iwapo mtu yuko Poland kwa njia halali au la lakini kina mtu ana haki ya kupata makazi ya heshima na chakula.

3476691

captcha