IQNA

Mufti Mkuu wa Croatia: Mkutano wa Umoja wa Kiislamu ni jukwaa la kuelezea hali ya nchi za Kiislamu

23:09 - October 20, 2021
Habari ID: 3474448
TEHRAN (IQNA)- Mufti Mkuu wa Waislamu wa Croatia amesema, Mkutano wa Umoja wa Kiislamu ni jukwaa la kuelezea hali ya sasa ya nchi za Kiislamu.

Sheikh Aziz Hassan Uvich ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Iran Press, ambapo mbali na kutoa shukrani kwa Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea pia tathimini yake kuhusu Mkutano wa Umoja wa Kiislamu kwa kusema, mikutano kama hiyo ni kiriri kwa maulamaa, wanafikra na wanasiasa kuzungumzia hali ya sasa.

Mufti Mkuu wa Waislamu wa Croatia ameeleza kwamba, kufanyika mikutano kama hiyo ni fursa mwafaka ya kupata uelewa wa hali ya nchi za Kiislamu na akaongezea kwa kusema "kadhia ya Palestina ni maudhui tunayoishuhudia tangu miaka na miaka nyuma hadi sasa; lakini mbali na kadhia hiyo, tunazungumzia pia nchi nyingine nyingi kama Afghanistan, Syria na Yemen ili kujua hali ilivyo katika nchi nyingine za Kiislamu."

Sheikh Aziz Hassan Uvich aidha amesema, kufanyika Mkutano wa Umoja wa Kiislamu na kuhudhuria waandishi wengi na vyombo mbalimbali vya habari katika mkutano huo kunafungua njia ya kujenga mawasiliano baina ya Waislamu na kupashana habari kuhusu hali ya nchi za Kiislamu.

Mkutano wa 35 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulianza jana hapa mjini Tehran kwa kaulimbiu ya "Umoja wa Kiislamu; Amani na Kuepukana na Mifarakano na Mizozo" kwa hotuba ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mkutano huo wa siku tano, ambao kwa sababu ya kuchunga miiko na miongozo ya kiafya ya kujiepusha na janga la corona unafanyika kwa mahudhurio ya moja kwa moja na kwa njia ya intaneti, unahudhuriwa na washiriki kutoka Iran na nchi 39 duniani.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Tuko katika siku tukufu za kuadhimisha Maulid ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad al Mustafa SAW, siku ambazo ni maarufu kama Maulidi. Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaadhimisha siku hiyo tarehe 12 Rabiul Awwal na Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanamini siku hiyo ni tarehe 17 Rabiul Awwal.

Miaka mingi iliyopita, Hayati Imam Khomeini MA, Kiongozi mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambaye binafsi alikuwa mstari wa mbele kulingania umoja wa Kiislamu alipendekeza kuwa, muda uliopo baina ya tarehe hizo mbili uwe ni "Wiki ya Umoja wa Waislamu" kwa lengo la kuimarisha mashikamano na udugu baina ya madhehebu za Kiislamu.

49067

captcha