IQNA

Rais wa Iran: Fikra ya kukurubisha madhehebu za Kiislamu ni ya kistratijia

16:28 - October 19, 2021
Habari ID: 3474444
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Iran amesema wazo la kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu lililobuniwa na Imam Khomeini (MA), Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni hatua ya kistratajia katika ulimwengu wa Kiislamu.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la 35 la Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hapa mjini Tehran leo Jumanne, Rais Ebrahim Raisi amesisitiza kuwa, suala la umoja linaweza kuwasilishwa kwa serikali za Kiislamu kwa kuepuka migawanyiko na taarifa zinazoweza kuibua mifarakano baina ya Waislamu.

Sayyid Raisi ameeleza kuwa, mfumo unaotawala dunia hautaki kuona umma wa Kiislamu ukiungana, na hivi sasa, baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wanautazama Uislamu kama kizingiti cha kufikia malengo yao.

Huku akiwakumbuka na kuwaenzi Meja Jenerali Qassem Soleimani na Ayatullah Mohammad Ali Taskhiri kutokana na jitihada zao za kisiasa na kielemu za kuondoa mifarakano na kuukurubisha pamoja umma wa Kiislamu, Rais Raisi amesema madola ya kibeberu yamebuni, kuyafadhili  na kuyapa silaha makundi ya kitakfiri kwa lengo la kuuparaganyisha umoja wa Waislamu duniani.

Ameeleza kuwa, mbali na kutumia makundi ya kigaidi na kitakfiri kuwagawa Waislamu katika misingi ya madhehebu, lakini ulimwengu wa Magharibi unatumia mbinu ya kupanda mbegu za chuki miongoni mwa Waislamu, na vile vile kusimika serikali dhaifu zitakazopigania maslahi ya Wamagharibi katika nchi za Waislamu, badala ya maslahi ya umma wa Kiislamu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Wamagharibi wameshindwa kufikia malengo yao, jambo ambalo limemfanya kijana wa Kiislamu ambaye huko nyuma alitamani kulia na kuishi katika mazingira ya Kimagharibi, hii leo anataka kuwa huru na kujikomboa.

Mkutano wa 35 wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza leo hapa mjini Tehran kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Umoja, chini ya kaulimbiu ya "Umoja wa Kiislamu; Amani na Kuepukana na Mifarakano."

Katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo, mbali na Rais Ebrahim Raisi, shakhsia wengine waliohutubu ni pamoja na Ziyad Nakhalah, Katibu Mkuu wa Jihadul-Islami ya Palestina, waziri mkuu wa zamani wa Iraq Adil al-Mahdi, Mufti wa Croatia Aziz Hasanvich, Mkuu wa masuala ya kimataifa wa Harakati ya Hamas Khalil al Hillah, Spika wa bunge la Algeria Bou Abdullah Bou Ghulamullah na wanafikra wengine kadhaa wa Ulimwengu wa Kiislamu.

Katika hafla hiyo ya leo kitazinduliwa pia kitabu cha Mawsuua'h cha majimui ya athari za Allamah Muhammad Taskhiri.../

4006238

captcha