IQNA

Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu wamalizika Tehran

17:36 - October 24, 2021
Habari ID: 3474463
TEHRAN (IQNA)- Kongamano la 35 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu limemalizika Jumamosi mjini Tehran baada ya kufanyika kwa muda wa siku tano.

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) Mohammad Baqir Qalibaf alikuwa mgeni wa heshima katika sherehe za kufunga kongamano hilo ambapo alisema ustawishaji umoja wa Kiislamu utawezesha ummah wa Waislamu  kufahamu kuwa, kwa mujibu wa mafundisho ya Qur’ani, shari kubwa kubwa ya kukabiliana nayo ni ukosefu wa uadilifu duniani pamoja na ubeberu.

Aidha ametoa wito wa kuwepo mazungumzo mapana baina ya nchi za Kiislamu ili kuimarisha umoja wa Waislamu na kukabiliana na makundi ya ukufurishaji, mifarakano na hitilafu.

Halikadhalika Spika wa Bunge la Iran ametahadharisha kuhusu njama za Marekani za kuibua vita vipya katika eneo.

Ameendelea kusema kuwa, nchini Afghanistan na eneo zima, kuna mikono iliyojificha ambayo daima inajitahidi kuchochea mifarakano kwa kuibua vita vya kimadhehebu. Jinai za hivi karibuni Afghanistan (kushambuliwa misikiti miwili ya Mashia wakati wa Sala ya Ijumaa) na njama za Marekani na Wazayuni zinazofanyika kwa lengo la kuibua ghasia Lebanon na Iraq, pamoja na mpango wa kuwachochea baadhi ya viongozi, yote ni mambo yanayofanyika ili kuibua vita kieneo.

Qalibaf amesema Marekani inaondoa askari wake katika eneo lakini bado inaendeleza njama za kuchchea fitina katika eneo hilo la Asia Magharibi.  Kuhusua kadhia ya Palestina, amesema  iwapo Waislamu wataungana, basi wanaweza kuwa na msimamo wa pamoja dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unakalia ardhi za Palestina kwa mabavu.

Mzungumzaji mwingine katika sherehe za kufunga kongamano hilo alikuwa ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu Hujjatul Islam Hamid Shahriari ambaye amewasilisha ripoti kuhusu kongamano la mwaka huu. Amesema wasomi, wanafikra, wanasiasa na wanazuoni zaidi ya 300 wameshiriki katika kongamano la mwaka huu ima kwa kuhudhuria katika ukumbi au kwa njia ya video.

Mkutano huo Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, ambao huandaliwa kila mwaka na Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu, ulianza Jumanne hapa mjini Tehran kwa kaulimbiu ya "Umoja wa Kiislamu; Amani na Kuepukana na Mifarakano na Mizozo" kwa hotuba ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mkutano huo wa siku tano, ambao kwa sababu ya kuchunga miiko na miongozo ya kiafya ya kujiepusha na janga la corona unafanyika kwa mahudhurio ya moja kwa moja na kwa njia ya intaneti, unahudhuriwa na washiriki kutoka Iran na nchi 39 duniani.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Tuko katika siku tukufu za kuadhimisha Maulid ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad al Mustafa SAW, siku ambazo ni maarufu kama Maulidi. Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaadhimisha siku hiyo tarehe 12 Rabiul Awwal na Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanamini siku hiyo ni tarehe 17 Rabiul Awwal.

Miaka mingi iliyopita, Hayati Imam Khomeini MA, Kiongozi mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambaye binafsi alikuwa mstari wa mbele kulingania umoja wa Kiislamu alipendekeza kuwa, muda uliopo baina ya tarehe hizo mbili uwe ni "Wiki ya Umoja wa Waislamu" kwa lengo la kuimarisha mashikamano na udugu baina ya madhehebu za Kiislamu.

4007371  

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha