IQNA

Nasrallah awataka Waislamu wadumishe umoja ili kukabiliana na maadui

17:08 - October 20, 2021
Habari ID: 3474446
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyed Hassan Nasrallah ametoa wito kwa Waislamu duniani kuungana ili waweze kukabiliana na njama za maadui.

Sayyed Nasrallah ameyasema hayo Jumanne alipohutubu kwa njia ya video katika ufunguzi wa Kongamano la 35 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu ambapo pia amepongeza kufanyika kila mwaka mkutano huo wa Umoja wa Kiislamu na kuutaja kuwa kati ya mafanikio ya mapinduzi ya Kiislamu.

“Ulimwengu wa Kiislamu umekuwa ukikabiliana na changamoto kadhaa kwa muda mrefu ambapo madola ya kibeberu na kiistikbari, yakiongozwa na Marekani, yamekuwa yakiwalenga Waislamu  lakini pamoj na hayo  baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran imechukua hatua za kuleta umoja baina ya Waislamu hasa kupitia kukurubisha madhehebu za Kiislamu,” amesema Sayyid Nasrallah.

Sayyid Nasrallah amesisitiza kuuhusu umuhimu wa kutumika mbinu mpya  za kuwakusanya wanazuoni wa Kiislamu kutoka maeneo yote ya dunia kwa ajili ya kubadilishana mawazo na uzoefu.

Mkutano wa 35 wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza leo hapa mjini Tehran kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Umoja, chini ya kaulimbiu ya "Umoja wa Kiislamu; Amani na Kuepukana na Mifarakano."

Mkutano huo hufanyika kila mwaka kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shia Ithanaashari linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

3476121/

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha