IQNA

Kiongozi Muadhamu Aonana na Washiriki wa Mashindano ya 27 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu

12:15 - July 16, 2010
Habari ID: 1956411
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Alkhamisi, Julai 15, 2010, ameonana na wahadhiri, majaji na washiriki wa Mashindano ya 27 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu mahfali ambayo imekwenda sambamba na maadhimisho ya siku alipozaliwa Imam Husain AS.
Mkutano huo umefanyika katika Husainia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) mjini Tehran. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika mkutano huo kwamba, Qur'ani Tukufu ni kamba na kishiko madhubuti cha Mwenyezi Mungu na amekumbusha kuwa, Qur'ani imetupa ahadi ya maisha mema na maisha hayo mema ni kuishi kwa heshima, usalama, ustawi, uhuru, elimu, maendeleo, maadili, upole na kusameheana chini ya mwavuli wa kuwa na ukuruba na mfungamano wa karibu sana na Qur'ani Tukufu na kushikamana vilivyo na kamba hiyo madhubuti ya Mwenyezi Mungu.

Mkutano na mahafali hayo yaliyojaa nuru yamefunguliwa kwa aya za Qur'ani Tukufu zilizosomwa na maqarii mabingwa na washindi wa tajwidi na tartili wa mashindano hayo ya 27 ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema katika mkutano huo kwamba, kuwa na mapenzi na mfungamano wa karibu na Qur'ani huandaa mazingira ya kupenya maarifa na uhakika wa Qur'ani katika nyoyo na nafsi za Waislamu.

Ameongeza kuwa, kwa miaka mingi kumekuwa na kampeni maalumu za kuzitenganisha nyoyo za Waislamu na Qur'ani na mafundisho yake matukufu kiasi kwamba katika baadhi ya nchi za Kiislamu, hata mlango wa jihadi umefungwa na hausomeshwi mashuleni kutokana na mashinikizo na kutaka kuwaridhisha maadui wa Uislamu.

Akifafanua zaidi kuhusu maisha bora na mema yaliyoahidiwa na Qur'ani Tukufu amesema, maisha hayo bora yanajumuisha maisha ya watu binafsi na ya jamii na roho na mwili wa mwanaadamu pamoja na dunia na Akhera yake.

Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesema kuhusu suala hilo kwamba, maisha bora yanayozungumziwa na Qur'ani Tukufu yanajumuisha pia ushuwari na utulivu wa roho, uhenezi, ufanisi, heshima ya kijamii na uhuru na istikilali ya uma ambapo utangulizi wa kufikia kwenye maisha hayo bora ni kufanyika jalsa na mashindano ya Qur'ani Tukufu na kulea mahufadhi na maqarii (watu wenye kuhifadhi Qur'ani na wasomaji wa tajwidi).

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amewausia vijana kujipinda katika elimu ya Qur'ani kwa kuzingatia maana yake na kuhifadhi aya zake zilizojaa nuru. Amekumbusha kuwa, kila mtu anapokaa na kusoma Qur'ani Tukufu, huelimika na hupungukiwa na ujinga na pia chemchemu mpya na nuru hububujika kwa ajili yake.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema, ni jambo muhimu sana kuwahamasisha na kuwashajiisha watoto wadogo na maborobaro kusoma, kuhifadhi na kuzingatia Qur'ani. Amesema kuhifadhi Qur'ani humpa fursa mwenye kuhifadhi kukariri mara kwa mara na kuzingatia aya zake na hivyo inabidi mwenye kuhifadhi Qur'ani ajue thamani ya neema hiyo kubwa inayopatikana katika kuhifadhi Qur'ani na asiruhusu neema hiyo ya Mwenyezi Mungu imtoke.

Vile vile amesema, kusoma Qur'ani kuanzia mwanzo hadi mwisho ni jambo muhimu na la dharura kabisa kwa ajili ya kuelewa maana ya Qur'ani na kuizoesha akili kuzingatia maana za aya za Kitabu hicho kitakatifu.

Ameongeza kuwa, maulamaa na walimu wa Qur'ani wanapaswa kubainisha kwa kina maarifa na mafundisho ya Qur'ani na kuwaondolea wapenzi wa Qur'ani Tukufu matatizo yote ya kufahamu aya za Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Udhma Khamenei amelinganisha harakati za Qur'ani nchini Iran kabla na baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na kukumbusha kuwa, katika kipindi cha miaka 31 iliyopita, Iran imeshuhudia harakati adhimu inayozidi kustawi katika upande wa kuzingatia Qur'ani Tukufu na kwamba wimbi kubwa la vijana kila leo linajiunga katika mkondo wa wasomaji na wataalamu wa Qur'ani Tukufu.

Mwanzoni mwa mkutano huo, Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadi, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala na msimamiaji wa Taasisi ya Wakfu na Mambo ya Kheri ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti kuhusu Mashindano ya 27 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya mjini Tehran na kusema kuwa, maqarii na mahufadhi 95 kutoka nchi 60 duniani wameshiriki katika mashindano hayo yaliyosimamiwa na majaji 14 wa kimataifa na wa Iran.

Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadi pia amesema, miongoni mwa ratiba zilizokwenda sambamba na mashindano hayo ni kongamano la kuwatukuza akinamama amilifu katika uwanja wa Qur'ani Tukufu na kongamano la makala za Qur'ani zilizojikita katika maudhui tatu za Qur'ani na Ahlul Bayt, Qur'ani na Muono Mpana pamoja na Qur'ani na Sayansi ya Jamii.

Vile vile katika mkutano huo, Dkt. Fajarullah Shadheli, mmoja wa majaji wa mashindano hayo kutoka Misri baada ya kusoma tajwidi mbele ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba fupi akitoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku alipobaathiwa na kupewa Utume Bwana wetu Muhammad SAW na vile vile kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku alipozaliwa Imam Husain AS.

Aidha ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa hatua yake ya kuzingatia na kuipa umuhimu mkubwa Qur'ani Tukufu.

Chanzo www.khamenei.ir
captcha