Taarifa ya wanazuoni hao imesema hatua hiyo ni sehemu ya njama chafu za kanisa dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Taarifa ya maulama wa Chuo Kikuu cha al Azhar imesisitiza juu ya udharura wa kufanyika jitihada za kuzima njama hizo na kusema kuwa hatua hiyo ya kanisa la Marekani itautumbukiza ulimwengu katika dimbwi la vita vya kidini.
Mufti wa zamani wa al Azhar Nasri Farid Wasil amesema kuwa hatua hiyo ya kanisa la Marekani ni sehemu ya hujuma ya makanisa ya Magharibi ya kueneza chuki na uhasama dhidi ya Uislamu. Sheikh Wasil amesema inasikitisha kuwa mpango huo ulianzishwa na Vatican miaka kadhaa iliyopita baada ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Benedict wa 16 kutoa matamshi yaliyoukebehi na kuuvunjia heshima Uislamu.
Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Mazungumzo Hamid al Rifai pia amesema kuwa watu wanaotoa wito wa kuchomwa moto kitabu kitakatifu cha Qur'ani hawana mfungamano wowote na dini za Uislamu, Ukristo wala Uyahudi na kwamba suala la kuzivunjia heshima dini za Mwenyezi Mungu linapaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kina.
Kwa upande wake mhadhiri wa teolojia katika Chuo Kikuu cha al Azhar Abdul Mu'ti al Bayumi amesisitiza kuwa wito wa kanisa la Florida huko Marekani wa kuchomwa moto Qur'ani Tukufu ni sehemu ya mpango wa kuwazingira Waislamu ndani na nje ya nchi hiyo. Amesema propaganda chafu dhidi ya Uislamu na kuifungamanisha dini hiyo na ugaidi ni tatizo sugu linalopaswa kutafutiwa ufumbuzi.
Ijumaa iliyopita kanisa la The Dove World Outreach Center of Gainesville huko Florida nchini Marekani liliwataka Wakristo kukumbuka siku ya Septemba 11 kwa kuchoma moto kitabu kitakatifu cha Qur'ani na kuitangaza siku hiyo kuwa ni 'siku ya kimataifa ya kuchoma moto Qur'ani'. 625845