Chuo Kikuu cha al Mustafa al Alamiyya kilichoko katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran kinatumia walimu wa kieneo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya Qur'ani Tukufu katika nchi ya Nigeria, suala ambalo limetajwa kuwa na mafanikio makubwa.
Hayo yamesemwa na msimamizi wa chumba cha Nigeria katika Maonyesho ya 18 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran Shuaib Muhammad na kuongeza kuwa Chuo Kikuu cha al Mustafa al Alamiyya kinafanya jitihada kubwa kueneza utamaduni na mafundisho ya Ahlul Bait (as) katika nchi mbalimbali duniani na kimepata mafanikio makubwa katika kutumia walimu wa kieneo kufundisha Qur'ani nchini Nigeria.
Muhammad Shuaib amesema hadi sasa chuo hicho kimefungua kituo cha Qur'ani na taaluma za kidini kwa lengo la kutoa elimu na mafundisho ya Ahlul Bait (as) katika mji wa Kano na kinakusudia kuanzisha chuo kingine kama hicho katika mji wa Abuja.
Akiashiria vitabu vya taaluma ya Qur'ani vinavyoonyeshwa katika chumba cha Nigeria katika Maonyesho ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran Shuaib ameongeza kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Nigeria kushiriki kwenye maonyesho hayo. Baadhi ya vitu vilivyoko katika chumba hicho ni nakala ya Qur'ani iliyoandikwa kwa hati za mkono, Qur'ani zenye umbo dogo zenye saizi tofauti, picha za Chuo Kikuu cha Qur'ani na Taaluma za Dini katika mji wa Kano, kitabu cha Raddul Adh'hani ila Maanil Qur'ani cha kadhi mkuu wa zamani wa Nigeria Sheikh Abubakr Mahmoud, tarjumi ya Qur'ani kwa lugha ya Hausa na kadhalika. 630446