IQNA

Jumuiya ya Ulimwengu wa Kiislamu yalaani kuainishwa Siku ya Kimataifa ya Kuchomwa Moto Qur’ani

15:40 - August 16, 2010
Habari ID: 1974797
Jumuiya ya Ulimwengu wa Kiislamu imetoa taarifa ikilaani vikali hatua ya kanisa la Kianglikana la Marekani ya kutangaza siku ya tarehe 11 Septemba kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuchomwa Moto Qur’ani Tukufu.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ulimwengu wa Kiislamu Abdullah bin Abdul Muhsin al Turki ametahadharisha katika taarifa hiyo juu ya taathira mbaya za hatua ya kanisa la Kianglikana la Florida nchini Marekani katika mahusiano ya kibinadamu, kuishi pamoja kwa amani, ushirikiano na maelewano kati ya mataifa mbalimbali.
al Turki amesema kuwa matamshi ya kebehi ya Kasisi Terry Jones, mkurugenzi wa kanisa la Dove World Outreach Center aliyesema kuwa “Uislamu ni dini ya shetani “ ni matamshi ya kichochezi na ya kiadui ambayo yataeneza chuki za kidini na vinyongo na kuwaumiza Waislamu kote ulimwenguni. Amesisitiza kuwa matamshi hayo yamezitia wasiwasi taasisi na jumuiya za Kiislamu.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ulimwengu wa Kiislamu amezitaka jumuiya na taasisi zote za Kiislamu nchini Marekani hususan Baraza la Uhusiano wa Uislamu na Marekani CAIR kukabiliana na mashambulizi na matamshi hayo ya kudhalilisha ya kasisi wa Kimarekani dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa kutumia sheria za Marekani kwenyewe na kuwazuia wafuasi wake ili wasichome Qur’ani Tukufu, jambo ambalo iwapo litafanyika litawakasirisha Waislamu kote duniani.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Kasisi Terry Jones Mkurugenzi wa kanisa la Dove World Outreach Centre katika jimbo la Florida nchini Marekani ametoa wito wa kuianishwa tarehe 11 Septemba kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuchomwa Moto Qur’ani. Kasisi huyo ni miongoni mwa wapinzani wakubwa wa dini ya Kiislamu nchini Marekani na amekuwa akiwachochea wafuasi wake kukabiliana na fikra za Kiislamu na kuchoma moto kitabu kitakatifu cha Qur’ani.
Ili kufanikisha lengo hilo, kasisi huyo ameanzisha ukurasa katika mtandao wa kijamii wa Facebook alioupa jina la ‘Siku ya Kimataifa ya Kuchomwa Moto Qur’ani’. 634267

captcha